Thursday, October 20, 2011

Kuropoka majaliwa

Kuropoka majaliwa, umakini wasojua,
Na hapo ndipo hutua, lisilofutika doa,
Mtu hujashangaa, tatizo kutolijua,
Kuropoka majaliwa, majuto ni mjukuu!

Dhahabu huitwa ukimya, kwa wale wanaojua,
Kinywa usipokifungua, ni mengi utayaambaa,
Ukijifanya wajua, na wengine huwa hua!
Kuropoka majaliwa,majuto ni mjukuu!

Waache wanaoongea, waongee wasojua,
Wewe uliyekomaa, hekima kuzingatia,
Eti hebu fikiria, neno shilingi lingekuwa?
Kuropoka majaliwa,majuto ni mjukuu!

Busara ni kunyamaa, vito kujikusanyia,
Onekana hujajua, lakini yote wajua,
Hili ukilizingatia, dunia utaijua,
Kuropoka majaliwa,majuto ni mjukuu!

Utakiwapo kutia, neno ndipo unapotia,
Hakuna kitakachopungua, kimya ukijikalia,
Ucheshi si kuongea, bali pia kutoongea,
Kuropoka majaliwa,majuto ni mjukuu!

Maneno huwa balaa, wambeya wanapojaa,
Dogo kubwa hujakua, hata kimo kuzidia,
Mengine kuvumilia, kazi kubwa kujakuwa,
Kuropoka majaliwa,majuto ni mjukuu!

Mshairi naongea, tokana na mazoea,
Viumbe ninawajua, wewe bado kuwajua,
Nafsi kutumikia, ndicho wanachokijua,
Kuropoka majaliwa,majuto ni mjukuu!

No comments: