Thursday, October 20, 2011

Ni miaka hamsini

Umeme uko ndotoni, maji wala siyaoni,
Wanambia hamsini, nifurahi kitu gani,
Mbavu za mbwa uwani, makazi yangu anwani,
Ni miaka hamsini, ndiyo nifurahi nini?

Sina thamni nchini, sithaminiwi duniani,
Heri nakaa mjini, wakoje wa vijijini?
Twafanyiana utani, haya wala hamuoni?
Ni miaka hamsini, ndiyo nifurahi nini?

Mboga yangu mgagani, utadhani klorokwini,
Bada yangu dizaini, nasaga mwangu nyumbani,
Lishe yangu majinuni, kaniruzuki Manani,
Ni miaka hamsini, ndiyo nifurahi nini?

Nikenda hospitalini, nichange kitu gani,
Najitibia nyikani, mwezi shilingi sioni,
Roho naweka rehani, wala hamjabaini,
Ni miaka hamsini, ndiyo nifurahi nini?

Niwalishe kitu gani, waendao skulini,
Utapiamlo kichwani, watafaulu somo gani,
Mlio madarakani, hebu shukeni chini,
Ni miaka hamsini, ndiyo nifurahi nini?

Wachina siamini, watupita kitu gani,
Ni kwenye mwaka sitini, wote tukiwa maskini,
Nasikia redioni, leo wanayo thamani,
Ni miaka hamsini, ndiyo nifurahi nini?

Malaysia nchi gani, na Korea kusini,
Tulipokuwa vitani, kulikuwa ni nyikani,
Wao nini wamebaini, watuacha maskini?
Ni miaka hamsini, ndiyo nifurahi nini?

Mtunzi nakuamini, kuyaweka shairini,
Ufikishe shaurini, sifurahii kwanini,
Waelewe yumkini, nchi ina mitihani,
Ni miaka hamsini, ndiyo nifurahi nini?

No comments: