Saturday, October 1, 2011

Hujifanya wanajua, waziibao fikira!

Nilipe kilicho bora, na mema kuniridhia,
Sina uzuri wa sura, wajihi ningenyanyua,
Niko chini kama chura, nalo lafaa kwa dua,
Hujifanya wanajua, waziibao fikira!


Naziogopa bakora, siku zikijatimia,
Isinikabili shura, malaika wakitua,
Wakanihoji izara, nilizozititimua,
Hujifanya wanajua, waziibao fikira!

Mimi sio mtu bora, hilo ama nalijua,
Ila naomba fikra, wengi zinazoongoa,
Nisikabili kwa ghera, hata nisiyoyajua,
Hujifanya wanajua, waziibao fikira!

Naomba kuwa ni jura, ya dunia nisiyojua,
Ukimya uwe dira, hata kwa ninayong'amua,
Na hasa penye hadhara, ya malimwengu kujaa,
Hujifanya wanajua, waziibao fikira!

Ninywe na nile fikra,na kiu kikaendelea,
Njaa isije kugura, tumbo wazi labakia,
Na kisha kwa maghufira, siache kunizindua,
Hujifanya wanajua, waziibao fikira!

Usinitie hasira, na ghadhabu kuingia,
Nisiwe mtu papara, kujifanya ninajua,
Nipe kilicho ijara,malipo yalotimia,
Hujifanya wanajua, waziibao fikira!

Mimi kiumbe uchwara, dharau nimezoea,
Najua si masihara,ndivyo mnavyodhania,
'Stakabiru 'stakibara'wewe tu nakusujudia,
Hujifanya wanajua, waziibao fikira!

Mimi hakika fukara,ila ulonipatia,
Nazikubali ishara,maamuma nimekua,
Na yangu kubwa biashara,kati yetu natambua,
Hujifanya wanajua, waziibao fikira!

Niruzuku uimara,kwalo nisijepotea,
Nimulike kwa munira,hata kunako ruia,
NIzawadie tiara,peponi inayoingia,
Hujifanya wanajua, waziibao fikira!

Nitunze njema fikra, za watu kuwasaidia,
Wasijepata madhara, kwa jambo kutolijua,
Unikabidhi bendera, njia kuwapasulia,
Hujifanya wanajua, waziibao fikira!

No comments: