Sunday, September 25, 2011

Mimi kwako ni mnyonge.

Mimi kwako ni mnyonge, ukipanda nnashuka,
Hakika mimi ni bwege, rahisi kudanganyika,
Isitoshe ni kikongwe, siwezi vita kutaka,
Hakika mimi mnyonge, salama yangu Rabuka!

Kwanini bure niringe, na huu wangu mzuka,
Si polio nijikinge, mama asipokumbuka,
Si ukimwi wanitenge, wasotaka kuumbuka,
Hakika mimi mnyonge, salama yangu Rabuka!

Si ugonjwa niugange, nisije kutaabika,
Hili ni la kwangu singe, kwalo nimebahatika,
Haiwezekani nivunge, fungate ilokamilika,
Hakika mimi mnyonge, salama yangu Rabuka!

Mjeshi naye achunge, na staha si hulka,
Kwa Mhehe ajinyonge, maudhi yakishindika,
Wenye kusepa wapange, kabla kuharibika,
Hakika mimi mnyonge, salama yangu Rabuka!

Mimi ni mnyonge, kushindwa nimeshindika,
Ila yangu niyalenge, sina la kubabaika,
Waache nje waringe, ya ndani ninayashika,
Hakika mimi mnyonge, salama yangu Rabuka!

Sina gele kwa wabunge, wala waliostahika,
Na matajiri nipunge, siwezi kukubalika,
Nawatafuta wanyonge, moyo wanaolainika,
Hakika mimi mnyonge, salama yangu Rabuka!

Sina jeuri ya kenge, kwa kuwa mamba ni kaka,
Siigizi ya madenge, ya kwangu yakishindka,
Kwa watu siombi tonge, kulala njaa naridhika,
Hakika mimi mnyonge, salama yangu Rabuka!

Wacha mizinga wachonge, shambani kuitundika,
Chora watupe vidonge,kisha vaja haribika,
Ona mbegu wazitwange, wakaja kuhamanika,
Hakika mimi mnyonge, salama yangu Rabuka!

Ya Ghaniyu unichunge, nisiwe wa kuropoka,
Miguu yangu ifunge, kwenye shari kutofika,
Na mkono uniunge, kwenye wema kuendeka,
Hakika mimi mnyonge, salama yangu Rabuka!

No comments: