Wednesday, September 21, 2011

Budi kuzaliwa upya, wewe wajivua gamba?

Chama changu kinatamba, kufanya liso jipya,
Chataka kujivua gamba, si kuzaliwa upya,
Ni wimbo wanaoimba,bila ya dira kuijua,
Budi kuzaliwa upya, wewe wajivua gamba?

Hawezi zaa mgumba, vipi wamtumainia,
Shahada hakiwi gumba, vipi utashahadia,
Taarabu sio rumba, huko si kutuharibia?
Budi kuzaliwa upya, wewe wajivua gamba?

Usiku hucha kwa komba, gizani nyendo ajua,
Riziki atazikomba, ghalani akazitia,
Utakuwa ni mshamba, ukija mwigilizia,
Budi kuzaliwa upya, wewe wajivua gamba?

Sio hai lako gamba, mara linshapwelelea,
Kwenye mizani ja pamba, hadhi yako inshakua,
Wazeeka wajiremba, nguchuro watahofia,
Budi kuzaliwa upya, wewe wajivua gamba?

Chama hakijawa gumba, hakijakoma kuzaa,
Vijana wanakipamba, wakosaje kukiinua?
Wazee kaeni chemba,umri umewazidia,
Budi kuzaliwa upya, wewe wajivua gamba?

Hakuna wa kumchimba, ni ukweli tunatoa,
Limechachamaa dimba, soka litatuengua,
Rijali tusipoomba, mechini kuja ingia,
Budi kuzaliwa upya, wewe wajivua gamba?

Kufumbua na kufumba, hatimaye kufungua,
Kalenda ya Muumba, haina wa kungojea,
Mwokozi kitindamimba, mziwanda hatofaa,
Budi kuzaliwa upya, wewe wajivua gamba?

Wewe wajivua gamba, badala kizazi kpya?
Ah, shangazi na wajomba,hamjioni mwaishia?
Kompyuta zawagomba,'facebook' yawazingua?
Budi kuzaliwa upya, wewe wajivua gamba?

Kashfa mnaziomba, na wengine kuzomea,
Siasa hizo za mtamba,fahali akimkataa,
Ubunfifu na ugumba,ni nani atavioa?
Budi kuzaliwa upya, wewe wajivua gamba?

Na dini mnaziomba,siasa kuwasaidia,
Huku wimbo mnaimba,udini unaingia?
Njaa yaua wajomba,hata makombo watwaa?
Budi kuzaliwa upya, wewe wajivua gamba?

Mahakama sasa jumba, siasa kuzikamia,
Polisi na jambajamba, chama kukisaidia,
Tunaitafuta kamba,kunyonga demokrasia,
Budi kuzaliwa upya, wewe wajivua gamba?

No comments: