Saturday, September 10, 2011

Ana deni la maisha

Anayeliiba wazo, wivi hajajiepusha,
Kila wazo lina mwanzo, na aliyeliumbisha,
Watu walio uozo, hili lawastaabisha,
Anayelipora wazo, ana deni la maisha.

Ama lao tangulizo, Mola linamkanusha,
Fikra wazibebazo, wakubwa kufurahisha,
Muumba yuko likizo, ha\wezi wababaisha,
Anayelipora wazo, ana deni la maisha.

Kama dubu wa igizo, tabia inatapisha,
Hanao huo uwezo, jipya kuvurumusha,
Kazi yao ya chombezo, ya wengine kufatisha,
Anayelipora wazo, ana deni la maisha.

Hupenda mazungumzo, pia kuzisoma insha,
Wapate yako mawazo, ndo waweze kuanzisha,
Makala uzitoazo, kusoma huhakikisha,
Anayelipora wazo, ana deni la maisha.

Hujiona mzomzo, wanapoyabahatisha,
Wakafanza micharazo,na ubingwa kujitwisha,
Madokta wa msazo,hugeuka wakapasha,
Anayelipora wazo, ana deni la maisha.

Hili kwangu si tatizo, hayo ni yao maisha,
Kilicho kwangu kikwazo, nasaba waziepusha,
Wamjue mwenye wazo, kumnukuu wabisha,
Anayelipora wazo, ana deni la maisha.

Hawahofu patilizo, Muumba kumkasirisha,
Hilo si lake agizo,hayo anayakanusha,
Haki lake angalizo,katika yetu maisha,
Anayelipora wazo, ana deni la maisha.

Ah, Bwana mwenye uwezo, bwana mwenye kulipisha,
Kuwa langu egemezo, kwa adili kunikosha,
Nisepe maangamizo, dunia hii ikiisha,
Anayelipora wazo, ana deni la maisha.

Wenye mali na uwezo, wajapo kujikausha,
Kunitenda kwa mabezo, yangu yakiwatajirisha,
Nipe ya kwako chelezo,nazidi kuniimarisha,
Anayelipora wazo, ana deni la maisha.

Waangaze wenye nazo, siha kuwatatanisha,
Na ajali mzomzo, zije kuwakaribisha,
Na siasa za uozo,wananchi kuja wachusha,
Anayelipora wazo, ana deni la maisha.

Na wasio na mawazo, wizarani kuwashusha,
Kizazi kiwe tatizo,yawasumbue maisha,
Dhahabu iwe uozo,na fedha kuwatapisha,
Anayelipora wazo, ana deni la maisha.

Waliokupua wazo, fadhila wakarudisha,
Wamiminie radhizo, katika yao maisha,
Watunukie na tunzo, uzidi kuwaimarisha,
Anayelipora wazo, ana deni la maisha.

Ahadi wewe tulizo, katika haya maisha,
Nirahisishie himizo, maagizo kufatisha,
Niokoe na mizozo, peponi kunijulisha,
Anayelipora wazo, ana deni la maisha.

No comments: