Monday, September 19, 2011

Madebe yanayovuja

Jaza maji litajaa, pipalo linalovuja,
Ila muda huchukua, ni pande mbili za mrija,
Vigumu maji kukaa, kwani lazima kuvuja
Madebe yanayovuja, jaza maji yatajaa.

Gumba katu hatazaa, hata umvalishe koja,
Mbilikimo hatokua, hiyo siyo yake siraja,
Mbinafsi si mjamaa, ukubwa kwake kufuja,
Madebe yanayovuja, jaza maji yatajaa.

Kubaleghe majaliwa, haliji kwa kila mmoja,
Watu wengi wanakua, kwa mwili si kwa hoja,
Utotoni wanabakia, hata wapande daraja,
Madebe yanayovuja, jaza maji yatajaa.

Kuvunja ungo hatua, si mwanamwali kwa wanja,
Kuropoka si kujua, heri ya mvuta ganja,
Na ajira kuikwaa, bado kwa watu si hoja,
Madebe yanayovuja, jaza maji yatajaa.

Watu wataka majaa, viongozi wenye chaja,
Matatizo kuwavua, wakaiona faraja,
Na fursa kuwapatia, wakazipanda daraja,
Madebe yanayovuja, jaza maji yatajaa.

Uongozi ni tabia, na uzuri sio hoja,
Kichwa kikitangulia, kilichokosa faraja,
Mafuu huwateua, wakaleta masihara,
Madebe yanayovuja, jaza maji yatajaa.

Wangapi wamesikia, ya Juja na maajuja,
Kuongoza makataa, dunia kuwa kioja,
Ndipo itakapoamuliwa, dunia kuwa mteja,
Madebe yanayovuja, jaza maji yatajaa.

Na debe huja kujaa, kisha huja kuvuja,
Raia watagharamia, viranjai wanaofuja,
Ni bara kwa Tanzania, hadi pia na Unguja,
Madebe yanayovuja, jaza maji yatajaa.

Viongozi tutapewa, wanaohitaji chaja,
Kama vile tumeishiwa, jamani fungeni mkaja,
Ni sinema ya sanaa, iko njiani inakuja,
Madebe yanayovuja, jaza maji yatajaa.

Hata nyanya zitapewa, ukubwa wenye vioja,
Wamiliki wa mkoa, wataonekana wakuja,
Na yatakayotokea, mkoa budi kuvuja,
Madebe yanayovuja, jaza maji yatajaa.

Nuru ikijaingia, wakazi sio waseja,
Haya watayakataa, na yote watayachuja,
Watapigania mkoa, uhuru wa kujikongoja,
Madebe yanayovuja, jaza maji yatajaa.

Ni kwa vipi Zanzibaa, leo eti twaitaja,
Ni nchi iliyokuwa, na rais kwao huja,
Na huku bara mkoa, viongozi ni wakuja?
Madebe yanayovuja, jaza maji yatajaa.

Ijiandae mikoa, miaka inayokuja,
Mkuu kumchagua, na sio wa kutajwa,
Kuwajibika ikawa, hiyo ndiyo yake hija,
Madebe yanayovuja, jaza maji yatajaa.

Naililia Tanzania, nchi yangu ya wakuja,
Kasahaulika mzawa, ni nani wa kumtaja?
Na vyeo wanaopewa, wakutugeuza mateja,
Madebe yanayovuja, jaza maji yatajaa.

Naililia Tanzania, nchi yangu ya viroja,
Juu, chini atakua, chini kupewa daraja,
Na ukoloni mpya, kwa utandawazi waja,
Madebe yanayovuja, jaza maji yatajaa.

Awali takabalia, kwingine tusende hija,
Amerika kutokua, njia yetu ya hijara,
Na Ulaya sio Maka, wala Madina siraja,
Madebe yanayovuja, jaza maji yatajaa.

Karima kwako twalia, tupe imara viranja,
Uchungu wanaojua, wa kubeba wetu mkaja,
Hapa watakaotutoa, twende kuliko faraja,
Madebe yanayovuja, jaza maji yatajaa.

No comments: