Saturday, September 10, 2011

Wakubwa wenye njaa

Wakubwa wenye njaa, kuua kwao si kazi,
Watu kwao ni dagaa,roho zetu wachuuzi,
Hawamwogopi Hafiizi,kiama wakikataa,
Kuua kwao si kazi, wakubwa wenye njaa!

Mutafifini machizi, mafuu na makataa,
Kichwani wanazo ndizi,sio akili nakataa,
Mioyo yao viazi,rojo iliyorojea,
Kuua kwao si kazi, wakubwa wenye njaa!

Usafiri kama kazi,unahitaji sheria,
Hata nao uchukuzi,viwango vinatakiwa,
Ila watu wapuuzi,nazi tumekwishakuwa,
Kuua kwao si kazi, wakubwa wenye njaa!

Viongozi wabarizi,na ndege wajipandia,
Wakulima na wakwezi,shaurienu mtajua,
Hatuiachii enzi,chini kufuatilia,
Kuua kwao si kazi, wakubwa wenye njaa!

Bandarini ni ajizi,rushwa inavyotembea,
Mtu akipewa andazi,chomboni hatoingilia,
Wakubwa na usingizi,mauti mwatuombea,
Kuua kwao si kazi, wakubwa wenye njaa!

Kwenye meli viokozi,nadra kufumania,
Hapana na vizuizi,Mola atuhurumia,
Hapana usimamizi,udhibiti ni hadaa,
Kuua kwao si kazi, wakubwa wenye njaa!

Wauaji si wanafunzi,walimu waliotimia,
Wabia wao viongozi,wote wanajichumia,
Na yao hayo machozi,ni mamba wanaolia,
Kuua kwao si kazi, wakubwa wenye njaa!

Wenye njaa viongozi,balaa limetushukia,
Dhaifu wafanyakazi, shilingi wanaopewa,
Huliachia jahazi,Muumba kuangalia,
Kuua kwao si kazi, wakubwa wenye njaa!

Hapanao wawekezi,malenga naulizia,
Meli zishehenezi,wingi kuja kupungua,
Abiria wabarizi,roho kutowakimbia,
Kuua kwao si kazi, wakubwa wenye njaa!

Au ubia mwagenzi, kwa nguvu kuzitumia,
Wakaiza wawekezi, manowari kutuletea?
Au sheria bazazi, watu wanazikimbiya?
Kuua kwao si kazi, wakubwa wenye njaa!

Wenzetu wape makazi,ya Manani ya Alaa,
Viongozi kwa kitanzi,cha isiyokwisha njaa,
Wala usiwape uzi,hawana la kujitetea,
Kuua kwao si kazi, wakubwa wenye njaa!

No comments: