Tuesday, October 25, 2011

Masika Uarabuni

Pengine hatufanani, lakini yanatufika,
Si wa nje si wa ndani, dunia yabadilika,
Upole unahaini, vijana wanacharuka,
Masika Uarabuni, rasharasha Afrika.


Wanapoteza imani, wale wasionufaika,
Hawaishi kwa karni, bahati nusu kufika,
Wasipopata auni, miaka haitafika,
Masika Uarabuni, rasharasha Afrika.

Wataka matumaini, na maisha ya hakika,
Wajue ni jinsi gani, waweza kusalimika,
Na kizazi chao njiani, huduma zahitajika,
Masika Uarabuni, rasharasha Afrika.

Maneno wamebaini, mfupa hutovunjika,
Na sasa wanasaini, tamko la kutikisika,
Asiyeleta pauni, mwenyewe ataondoka,
Masika Uarabuni, rasharasha Afrika.

Kazini na mahuleni, wote wameshastuka,
Hawataki ya uani, wanataka ya hakika,
Fisadi kaeni chini, vipi watapoozeka?
Masika Uarabuni, rasharasha Afrika.

Na wazazi majinuni, lao halitakubalika,
Wachekwa wa zamani, uoga umewazunguka,
Haya ni maisha gani, wakataa kukubalika,
Masika Uarabuni, rasharasha Afrika.

Vipi wajipa thamani,hakuna linalofanyika,
Mijini na vijijini, kizazi kinataabika,
Huu uongozi gani, watu wasiponeemeka,
Masika Uarabuni, rasharasha Afrika.

Wakubwa wajidhamini, hata wasipohusika
Wake wawathamini, na ahali waliozalika,
Laki si baki yakini, na hao sio shirika,
Masika Uarabuni, rasharasha Afrika.

Apartheid wadhani, sasa hapa yafanyika,
Wapo wanaojidhani, wao wa kuthaminika,
Na wengine maaluni, na hawatohesabika,
Masika Uarabuni, rasharasha Afrika.


Mtunzi nabaini, hofu nimeiandika,
Lakini haya yakini, ndiyo yanayofanyika,
Kama kukosa amani, chimbuko linachimbuka,
Masika Uarabuni, rasharasha Afrika.

No comments: