Monday, October 24, 2011

Watu hawana thamani

Watu hawana thamani

KAMA ilivyo Ulaya, sasa yazuka nyumbani,
Vitu vinaabudiwa, mtu hanayo thamani,
Mavazi usipong'aa, waonekana ni duni,
Vitu vinathaminiwa, watu hawana thamani!

Ni ibada pia dua, vitu vilo madukani,
Na hija yakubaliwa, kwenda vileta makani,
Navyo ukipungukiwa, waonekana afkani,
Vitu vinathaminiwa, watu hawana thamani!

Mapambo nje twajua, sio usafi wa ndani,
Hili nikiimanishia, ya rohoni na moyoni,
Nyikani tunapotea, twadhani njia twajua,
Vitu vinathaminiwa, watu hawana thamani!

Tumetekwa Tanzania, na bepari duniani,
Wanataka sisi kua, kama walivyo Marekani,
Na uchi tutatembea, hili ninayo yakini,
Vitu vinathaminiwa, watu hawana thamani!

Si watu wanaojijua, viongozi wetu nchini,
Waamka na kutembea, siraji hawaioni,
Tunazidi kupotea, maendeleo wadhani,
Vitu vinathaminiwa, watu hawana thamani!

Ningelitoa usia, niseme baniyamini,
Furaha ndani yakaa, huipati mitaani,
Na havitakupatia, vitu ukijaza ndani,

Raha Allah Kumjua, si mali wala madini,
Juu, chini huja huwa, sheria ya duniani,
Kubwa, dogo huja hua, na hili nalo yakini,
Vitu vinathaminiwa, watu hawana thamani!

Kizuri huwa kibaya,chema kukosa thamani,
Akili huja sinyaa, akiridhia Manani,
Fahari hukutumbukia, ukiipuuza dini,
Vitu vinathaminiwa, watu hawana thamani!

Mola nakuangukia, dunia nisithamini,
Viumbe kushikilia, hata kama maskini,
Kisha nikawasaidia, 'shara yara dharatini',
Vitu vinathaminiwa, watu hawana thamani!

No comments: