Sunday, October 23, 2011

Nchi isiyoshinda

Ninawaonea gele, nchi zenye washindani,
Wasio na makelele, bali zina ushindani,
Ni nchi isiyoshinda, kila fani inashindwa!
Ni nchi isiyoshinda, kila fani inashindwa!

Si wazima bali mwele, twaugua akilini,
Imezimika miala, ya wa kweli ushindani,
Yamebaki makelele, tv na redioni,
Ni nchi isiyoshinda, kila fani inashindwa!

Zinshanicheza chale, Yanga, Simba siamini,
Hawa ndio walewale,nje giza nuru ndani,
Kimataifa bwelele, chakula chao wageni,
Ni nchi isiyoshinda, kila fani inashindwa!

Ushabiki niagule, umekufa ja moyoni,
Nafsi nikomalile, wakaya sina utani,
Ngoma sijui shinale, nikacheze kitu gani?
Ni nchi isiyoshinda, kila fani inashindwa!

Hawa si watu wanole, kupanga si yumkini,
Mambo yaenda kikole, utadhani wa zamani,
Na siasa zipalile, sangari nishabaini,
Ni nchi isiyoshinda, kila fani inashindwa!

Ni nchi ya wanawale, wazaliwao njiani,
Kaulizile babale,utaambiwa yumkini,
Mwanaharamu kalole, na herufi habaini,
Ni nchi isiyoshinda, kila fani inashindwa!

Ni nchi ya mashogale, wanaume siwaoni,
Mhehe ningefyale, huu ni mchezo gani,
Si filimbi si kengele, hamnao ushindani,
Ni nchi isiyoshinda, kila fani inashindwa!

Neno langu lile lile, sibadiliki abadani,
Vyombo vya habari ngole, wawashinda uwanjani,
Wastahiki kilele, au kadi za kijani?
Ni nchi isiyoshinda, kila fani inashindwa!

Lelemama wafanyale, hawa si watu makini,
Hata ngoma wateule, huingia shindanoni,
Mazoezi toka kale, ndio njia ya yakini,
Ni nchi isiyoshinda, kila fani inashindwa!

Na wazawa washikile, bendera kwa kila fani,
Ni makocha wateule, na walimu wa kanuni,
Hali hii wailole, na tupige abautani,
Ni nchi isiyoshinda, kila fani inashindwa!

Viwanja tuezekele, mijini na vijijini,
Tuvitunze si ndulele, viwe rangi ya kijani,
Na maji tuyafosile, ghali hayapatikani,
Ni nchi isiyoshinda, kila fani inashindwa!

Mipango tuipangile, sio kungoja mwakani,
KIla mchezo uvale, tarehe za ushindani,
Tusiwe ni misukule, twasukumwa viwanjani,
Ni nchi isiyoshinda, kila fani inashindwa!

Wanasiasa walole, uchumi ukiwa duni,
Na michezo hudumale, maktaimu kuauni,
Michezo haiendi mbele, nyuma hubaki yakini,
Ni nchi isiyoshinda, kila fani inashindwa!

No comments: