Sunday, October 2, 2011

Nchi hii yetu sote

Yetu sote nchii hii, sio ya mtu mmoja,
Mchana na asubuhi, jumla si rejareja,
Tena tunawakinai, wanaojifanya waja,
Nchi hii yetu sote,sio ya chama kimoja!

Hisa zetu tanbihi, kila mtu kura moja,
Hao wanaojidai, eti sisi ni wakuja,
Twawaambia wazirai, kiama chao kinakuja,
Nchi hii yetu sote,sio ya chama kimoja!

Hamsini inadai, miaka waliofuja,
Watatupa ipi rai, kama wao si mateja,
Hata wasiotanabahi, hawaioni faraja,
Nchi hii yetu sote,sio ya chama kimoja!

Ukiritimba nishai, watu kazi kubwabwaja,
Misingi hawaijui, kanuni zao za kuja,
Na filimbi na nai, wadhani nazo zina hoja,
Nchi hii yetu sote,sio ya chama kimoja!

Wapemba na Waunguja, Waha na Wamasai,
Wamakonde na Wangazija, na wote tuliowahi,
Hakuna mtu wa kuja,sote ni raia hai,
Nchi hii yetu sote,sio ya chama kimoja!

Hakika kila mmoja, awezalo tumstahi,
Isiwe twaua umoja,kwa kudai hawafai,
Vikome navyo vioja,watoto kuwa warithi,
Nchi hii yetu sote,sio ya chama kimoja!

Tujengeni madaraja, ili sote tufurahi,
Budi kuwa na umoja, wakweli si wa maslahi,
Tuukimbie useja, na tando za baibui,
Nchi hii yetu sote,sio ya chama kimoja!

Hatuna muda wa kungoja, tuogope makarai,
Nchi kupanda daraja, mapinduzi inadai,
Wachapa kazi kutaja,na si wangoja chai,
Nchi hii yetu sote,sio ya chama kimoja!

Tutajengaje umoja, na wakubwa hawafai?
Tutapandaje daraja, watu kazi hawajui?
Udugu sumu ya umoja, makapi huwa adui,
Nchi hii yetu sote,sio ya chama kimoja!

Uswahiba wa lahaja, hakika huu jinai,
Jamaizesheni mrija,ukiyabeba makarai,
Inachosha ngojangoja,hasadikiki ndugu mui,
Nchi hii yetu sote,sio ya chama kimoja!

No comments: