Monday, October 31, 2011

Niuzieni kijiji

Nanena kama kuuza, kweli ndiyo yenu kazi,
Kijiji nawajuuza, nitafanya manunuzi,
Watu mkishawapuuza, ninapenda hiyo kazi,
Niuzieni kijiji, ili chote kiwe changu!

Madalali napuuza, nawaombeni wajuzi,
Msije kuja niiza, wala kufanya ajizi,
KIfedha ninajiweza, ardhi nataka hodhi,
Niuzieni kijiji, ili chote kiwe changu!

Ni mtu wa kuwekeza, kama hamjamaizi,
Na simwamini Pweza, hata atoke Uholanzi,
Nai nitaipuliza, naye awe hajiwezi,
Niuzieni kijiji, ili chote kiwe changu!

Mchezo wangu hucheza, waroho na walanguzi,
Na hata wasiojiweza, siwapi na siwatunzi,
Thawabu kulimbikiza, mengineyo upuuzi,
Niuzieni kijiji, ili chote kiwe changu!

Jua chungwa sio chenza, ingawa mmoja mzazi,
Wasemao nimeoza, sina ila maombezi,
Laniogopa jeneza, na nyie hamniwezi,
Niuzieni kijiji, ili chote kiwe changu!

Ukubwa ninauweza, kwani wengine washenzi,
Sio kazi kuongoza, mbona nina mwingi ujuzi,
Trilioni ukichuuza, utashindwa na vibuzi?
Niuzieni kijiji, ili chote kiwe changu!

Waandishi nawakweza, ninaifanya palizi,
Watu wasiojiweza, kuukata siwakwazi,
Kwangu mchuzi wa pweza, vitafunwa na mandazi,
Niuzieni kijiji, ili chote kiwe changu!

Huanza kwa kuyauza, mashamba ya wanagenzi,
Kisha watafululiza, kuuza hata makazi,
Na mwishowe huweza, kuwauza vijakazi,
Niuzieni kijiji, ili chote kiwe changu!

Wanajifunza kuuza, hiyo ndiyo yao kazi,
Tena vya wengine huuza, vyakwao hawaviuzi,
Si shaibu si ajuza, hubaki kwenye simanzi,
Niuzieni kijiji, ili chote kiwe changu!

Mie ninaitanguliza, nia yenye uwokozi,
Kijiji mkikiuza, iwe kwangu mnunuzi,
Kisha wote nitafunza, wajue shika mianzi,
Niuzieni kijiji, ili chote kiwe changu!

Mianzi wataicheza, kwa muziki wa mahadhi,
Ya moyoni hawataviza, wataacha waziwazi,
Ngoma hamtaibeza, na kucheza hamuwezi,
Niuzieni kijiji, ili chote kiwe changu!

Nyumba tutatengeneza, kwa makuti na mabanzi,
Kodi nitakayotoza,ni huruma na mapenzi,
Gharama ni mangimeza,na waongo waenezi,
Niuzieni kijiji, ili chote kiwe changu!

Nitalindoa giza, kwenye nuru wabarizi,
Juu nitawaongoza, wazipande hizo ngazi,
Wataweza wasichoweza, kwa rehema na majazi,
Niuzieni kijiji, ili chote kiwe changu!

Watajua nani funza, na nani ni kiongozi,
Ufukara watasaza, wakiona mbalamwezi,
Atue kifimbo cheza, na bakora kuienzi,
Niuzieni kijiji, ili chote kiwe changu!

Ushuru sitautoza, kwa kaniki na viazi,
Vipi utawaunguza, motoni wenye makazi,
Laana nitaichagiza, hata kwenye usingizi,
Niuzieni kijiji, ili chote kiwe changu!

Milki nitatangaza, ni marufuku kwa wezi,
Fisadi nitawangaza, watunukiwe vitanzi,
Wanasiasa sikiza, ngoma hii hamuwezi,
Niuzieni kijiji, ili chote kiwe changu!

Viongozi kwenye giza, mtayavuna masinzi,
Mshindwao kuongoza, chini mpate makazi,
Njia wanaotengeneza, tutawapatia kazi,
Niuzieni kijiji, ili chote kiwe changu!

No comments: