Monday, October 10, 2011

Yuko wapi shujaa wa Afrika?

Twamsaka Afrika, yuwapi wetu shujaa,
Awezaye kuzizika, kasumba za kutawaliwa,
Na asiyeterereka, na njia anayejua,
Yuwapi wetu shujaa, tumfate Afrika!

Nchi zatia wahaka, kulogwa tunadhaniwa,
Na viongozi mizuka, ndio wanatuzingua,
Wakipangwa na mahoka, hawaoni hata njia,

Cheoni wababaika, wanashindwa kuamua,
Msukule watukuka, nao ukiwalingania,
Ulaya na Amerika, ndiko unga wanapewa,
Yuwapi wetu shujaa, tumfate Afrika!

Nafasi wamezishika, na vyote wang'ang'ania,
Hata vyoo wanashika,vigumu kuviachia,
Wengine wanatucheka,limbukeni tulivyokua,
Yuwapi wetu shujaa, tumfate Afrika!

Kila jamba tunataka, peke yetu kuamua,
Mabingwa walalamika, wanasesere wamekua.,
Na uzee ukifika, hatutaki kuyatua,
Yuwapi wetu shujaa, tumfate Afrika!

Vijana wa Afrika, sasa wanatuzomea,
NI mbali tulikotoka, na hatujapiga hatua,
Wana makubwa mashaka, kama tutawakomboa,
Yuwapi wetu shujaa, tumfate Afrika!

Vinginevyo wanataka, taifa kulichukua,
Ili tuweze kuvuka,tulikoishaazimia,
Na kulipia sadaka, tuloacha kutoa,
Yuwapi wetu shujaa, tumfate Afrika!

Tubadilike haraka, si magamba kujivua,
Watu wapya tunataka, na nchi mpya kuvumbua,
Hili halina wahaka, mwapaswa kulisikia,
Yuwapi wetu shujaa, tumfate Afrika!

Vinginevyo ni gharika, mkae mwategemea,
Hairudi Afrika, nyuma ilikotokea,
Mbele budi kuendeka, ima-fa-ima pigaua,
Yuwapi wetu shujaa, tumfate Afrika!

Kilichobaki hakika, kujitokeza shujaa,
Mjini anakotoka, kijijini kuingia,
Ikaanza kupangika, ufukara kukataa,
Yuwapi wetu shujaa, tumfate Afrika!

Kwanza hatotajirika, ila wa kwake raia,
Nao wakishajengeka, naye atajiinua,
Hapo ndipo Afrika, kumekucha itakua,
Yuwapi wetu shujaa, tumfate Afrika!

No comments: