Tuesday, October 18, 2011

Mo Ibrahim

Kama kasi ndio hii, kuipata tunzo kazi,
Tuamke asubuhi, kuifanza fumanizi,
Mipango tuisanii, na mikakati kuenzi,
Mo Ibrahim kazi, kama kasi ndio hii.


Nchi yetu majeruhi, siasa zenye vitanzi,
Mitego twaikinai, wamezidi viongozi,
Ujanja mtu kuwahi, na wachache wa vitenzi,
Mo Ibrahim kazi, kama kasi ndio hii.

Matatizo hatujui, kwisha hupanda ngazi,
Pia rushwa haifai, hutia jicho kibanzi,
Na waudhi usanii, hata pia kwa Mwenyezi,
Mo Ibrahim kazi, kama kasi ndio hii.

Matatizo tukinai, kama wizi na ujambazi,
Haki hatuitumii, dhuluma tunaienzi,
Vijiji tuvistahi, vipate bora majenzi,
Mo Ibrahim kazi, kama kasi ndio hii.

Fursa tuzisabahi, za kiuchumi kumaizi,
Watu hamasa wadai, toka kwao viongozi,
Viwanda na ustawi, kila mtu apate kazi,
Mo Ibrahim kazi, kama kasi ndio hii.

Penye mbao natanabahi, kweli hakuna wajenzi,
Niitoe ipi rai, pawe na watangulizi,
Na tanzu za baibui, machoni zimeshajizi,
Mo Ibrahim kazi, kama kasi ndio hii.

Kasi isiwe ya chui, bali ya duma mkwezi,
Watu wanayo madai, kuyajibu tumaizi,
Ahadi hazitufai, tukishaenda kwa Mwenyezi,
Mo Ibrahim kazi, kama kasi ndio hii.

Tufaidi leo hii, kama hao viongozi,
La sivyo tunawarai, vipi hamuipunguzi,
Mishahara asubuhi, kwani kazi hamuwezi?
Mo Ibrahim kazi, kama kasi ndio hii.

Kila kitu ni nishai, sasa twazua majizi,
Vijana wa nchi hii, ajira kwao ni kazi,
Mikakati hatujui, kuondoa jinamizi,
Mo Ibrahim kazi, kama kasi ndio hii.

Wallahi hatujitambui, kama vile mabazazi,
Urithi wa nchi hii, unatosha kwa majenzi,
Ila tunayo nakisi, hawatimu viongozi,
Mo Ibrahim kazi, kama kasi ndio hii.

Vinara hawatufai, umaskini waenzi,
Ukwasi wakiuwahi, kutukumbuka ajizi,
Wabunge ni wasanii, majimbo yao hawaenzi,
Mo Ibrahim kazi, kama kasi ndio hii.

Mikoani twastahi, wakupewa viongozi,
Mimi natoa rai, kuchagua sio kazi,
Tuwe na vinara hai, mkoani kwa mageuzi,
Mo Ibrahim kazi, kama kasi ndio hii.

Mikoa uchumi hai, madaraka tuienzi,
Tusiifanye makarai, maji machafu kuhodhi,
Nchi ipate stawi, wawe huru viongozi,
Mo Ibrahim kazi, kama kasi ndio hii.

Nchi haiwezi stawi, mikoa tusipoenzi,
Ushindani kuudai, ni kitu chenye majazi,
Kubwa sana nchi hii, hatuhitaji wapagazi,
Mo Ibrahim kazi, kama kasi ndio hii.

Kama kasi ndio hii, mikoa hatutangulizi,
Nchi huja kuzirai, miundo ipate ganzi,
Viungo kama havifai, mwili hautavienzi,
Mo Ibrahim kazi, kama kasi ndio hii.

Ukiritimba haufai, yatakwama mageuzi,
Hii ni kubwa jinai, umma katu hauenzi,
Na vingi vya nchi hii, hiki kikubw kitanzi,
Mo Ibrahim kazi, kama kasi ndio hii.

No comments: