Thursday, October 20, 2011

Mnafiki

ZABIBU kumbwaga chini, sungura kasema mbichi,
Waona ajabu gani, kusema kichwa kibichi,
Kwani wao watu gani, bali za shamba kabichi,
Mnafiki twamjua, sungura kasema mbichi!

Yanga, simba uwanjani, atasema mshindwa mechi,
Kwa aliye taabani, tuhuma hawaifichi,
Binadamu mbaini, tabia humweka uchi,
Mnafiki twamjua, sungura kasema mbichi!

Na msemwa haamini, na kauli hachekechi,
Mbovu na puya zi ndani, mtalishwa wali mbichi,
Kisingizio kitu gani, nani kawafundisha nachi?
Mnafiki twamjua, sungura kasema mbichi!

Jumbe niache makani, na polisi wasinisachi,
Kaniudhi majinuni, kaiba zangu chikichi,
Kanifanyia uhuni, si wake mchikichi,
Mnafiki twamjua, sungura kasema mbichi!

Watazame limbukeni, akikaa kwenye kochi,
Raha akiibaini, usingizi haumwachi,
Kazi kumtoa ndani, TV ikiwa na mechi,
Mnafiki twamjua, sungura kasema mbichi!

Miaka nimesaini, si ya kwangu hii nchi,
Wenyewe ni lalwamani, apendwa bora Mdachi,
Mweusi alwatani, mkoloni nusu-uchi,
Mnafiki twamjua, sungura kasema mbichi!

Na walio mashakani, chuki zao hawafichi,
Utapandaje paani, ngazi uipige tanchi,
Juha nakaa tawini, kwanguka chini siwachi,
Mnafiki twamjua, sungura kasema mbichi!

Katwaa kinu uwani, kauacha ndani mchi,
Utatwanga na nini, au ni mzee wa panchi?
Ufanyalo siamini, utaacha kuwa kuchi,
Mnafiki twamjua, sungura kasema mbichi!

Kama u mtu makini, tulia utunze ranchi,
Na wakija kijijini, wajukuu wape pochi,
Mjini sasa nyikani, na kwako kucha haukuchi,
Mnafiki twamjua, sungura kasema mbichi!

Mshairi masikini, mbivu siiti mbichi,
Ukweli nilishabaini,haukuwa nusu uchi,
Bayana niliamini, kufika kipindi hichi,
Mnafiki twamjua, sungura kasema mbichi!

No comments: