Saturday, October 1, 2011

Wazo liko kama mbegu, huweza ota likafa!

Kama dengu au kungu, wazo halina pa kushika,
Yafaa kutunza mbegu,pale isipopandika,
Chunga isioze njugu,kuota haitatweta,
Wazo liko kama mbegu, huweza ota likafa!

Wachunguze kina ndugu,wepesi wa kuokota,
Wazo huja wanguwangu,kisha wao kukamata,
Hawaulizi kifungu,wala hoja kutafuta,
Wazo liko kama mbegu, huweza ota likafa!

Hawajaijua mbegu,mara wanaipepeta,
Wataipanda kwa ndugu,mahala isipoota,
Hujifia kwa uchungu,au ikajazorota,
Wazo liko kama mbegu, huweza ota likafa!

Wazo labeba utungu,mzawa aliyelipata,
Na haya sio majungu,nakupa kisicho tata,
Sifichi kwenye uvungu,mie si mtu wa matata,
Wazo liko kama mbegu, huweza ota likafa!

Nakuepusha na rungu,usije nundu kuota,
Mkunjufu moyo wangu,japo haujatakata,
Hakika zako ni zangu,mradi unanifuata,
Wazo liko kama mbegu, huweza ota likafa!

Wevi haki ni ukungu,njia hawataipata,
Wanamkosea Mungu,malaika wawasuta,
Washindwa naye Mzungu,ukoloni aliyesita,
Wazo liko kama mbegu, huweza ota likafa!

Akheri ya nungunungu,yakini nimeipata,
Kuliko ya ndugu yangu,Mwafrika wa Msata,
Hujidai ni Mzungu,kumbe kwa haki mkata,
Wazo liko kama mbegu, huweza ota likafa!

Tuko huru twatokota, na wapishi si wazungu,
Ni akhali wanang'ata, kama mavu na nyigu,
Na mikia twafyata, walivyo wakali njagu,
Wazo liko kama mbegu, huweza ota likafa!

Hakuna kinachoota, zinaharibika mbegu,
Ugumba unatusuta,mimi pia na wenzangu,
Kipi chetu kinapeta,ila sadaka za Mungu?
Wazo liko kama mbegu, huweza ota likafa!

Tunashindwa matrekta, kuunda kisa mizungu,
Barabarani Toyota,gari lako, gari langu,
Nini chetu kimeota,ila wizi na majungu,
Wazo liko kama mbegu, huweza ota likafa!

Utasa unatuteta, wazazi pia na ndugu,
Kuunda tumetokota, twaagiza vya wazungu,
Kisha eti tunateta,dunia ya pili fungu?
Wazo liko kama mbegu, huweza ota likafa!

No comments: