Monday, October 31, 2011

Magari maendeleo

Vigelegele watoto, magari maendeleo,
Hii kubwa yenu ndoto, kwa yale myatakayo,
Twawapa huu uoto, myajenge matamanio,
Magari maendeleo, dhana mpya Tanzania.

Hata bila ya kipato, yaweke matarajio,
Mbona haya ni mchoto, usihofu mwanakwao,
Ukishindia ruketo, bado unalo gawio,
Magari maendeleo, dhana mpya Tanzania.

Ni haki yako mtoto, gari ni la kwako gao,
Baba hakupigi ngoto, yeye na mama la kwao,
Babu na bibi si ndoto, pia kuwa na kipandio,
Magari maendeleo, dhana mpya Tanzania.

Hata pasipo vipito, tunataka matokeo,
Kwenye tope si kokoto, haya ni maendeleo,
Na pasipo zimamoto, kuna bima yako ngao,
Magari maendeleo, dhana mpya Tanzania.

KIna Kurwa kina Doto, hii ni dunia yao,
Acheni malipyoto, ya kitoto madai yao,
Ni kipi chenye mvuto, kwenye maendeleo?
Magari maendeleo, dhana mpya Tanzania.

Ni kipi chenye mvuto, kwenye maendeleo,
Kulikoni kaamoto, Japani tununuayo,
Motokaa za Kyoto, Uchina pia Tokyo,
Magari maendeleo, dhana mpya Tanzania.

Tumezitimiza ndoto, ndani wapo walalao,
Ni viota vyenye joto, kwa wote wapendanao,
Si makaburi mazito, vibaya watumiao,
Magari maendeleo, dhana mpya Tanzania.

Nyumba hazina mapato, hujanjaruka waishio,
Budi kuwapa mseto, na ajira bila mafao,
Zifutike zao ndoto, magari yawe ni yao,
Magari maendeleo, dhana mpya Tanzania.

Kwa mkopo mikong'oto, huisha jeuri yao,
Wawe kama ni watoto, rambaramba iwe yao,
Na wakishindwa makato, ukata uwe ni wao,
Magari maendeleo, dhana mpya Tanzania.

Chakula kimchakato, hutunza afya yao,
Wataliongeza joto, zirudi akili zao,
Hvi yafanye mpito, haya yasiwe ni yao,
Magari maendeleo, dhana mpya Tanzania.

Ajali zipate uzito, kukata maisha yao,
Nyota ya kijani keto, kucheza mchezo wao,
Hati hii hati ya mkato, huibua yaeleayo,
Magari maendeleo, dhana mpya Tanzania.

Yende hadi Kibongoto, Siha hadi Rahaleo,
Yawazuzue Mporoto,wao na vizazi vyao,
Nguo zisiwe misuto, mitumba ni hadhi yao,
Magari maendeleo, dhana mpya Tanzania.

Magari ni manukato, maua yachanuayo,
Hulea hawa vizito, maboya ya sera zao,
Kwa karatasi uzito, huwa ndiyo deni lao,
Magari maendeleo, dhana mpya Tanzania.

Tanzania mtokoto, ni wengi yawasumbuao,
Hivyo vyombo vyenye moto, na njiani vituko vyao,
Pikipiki na mkokoto, ni wengi waumiao,
Magari maendeleo, dhana mpya Tanzania.

Ipepeteze pepeto, pumba na chuya ziwayo,
Wahitaji na kung'uto, kwa haya uyachujayo,
Ukubwa kana utoto, malezi hayana mwao,
Magari maendeleo, dhana mpya Tanzania.

Naufanya mchakato, historia jana, leo,
Unapoangaza moto, kwa jotole na baridiyo,
Samaki wangu ni sato, sangara si kitoweo,
Magari maendeleo, dhana mpya Tanzania.

No comments: