Monday, October 3, 2011

Ameshajilimbikizia

Ameshajilimbikizia, fisadi kushindwa kazi,
Nchi keshawauzia, wa jana pia wa juzi,
Raia hawathamini, nchi keshafanya uchuzi,
Ameshajilimbikizia, fisadi hawezi shindwa.

Ndio wanaotufua, kwa maganda ya viazi,
Wanaotumiminia mafuta ya maandazi,
Mgongo kuutumia, wa chupa mafuta nazi,
Ameshajilimbikizia, fisadi hawezi shindwa.

Pasi weshajipigia, suruali kama ngozi,
Njiani wakitembea, nawakumbuka manazi,
Nchi inakoelekea,imeanza panda ngazi,
Ameshajilimbikizia, fisadi hawezi shindwa.

Ukuu huukimbilia, japo hawawezi kazi,
Mamlaka wakichukua, nchi hushikwa maradhi,
Na daima huugua, dawa hazifanyi kazi,
Ameshajilimbikizia, fisadi hawezi shindwa.

Ni chama huwachagua, kinachotuchuna ngozi,
Wachache wanaosaidiwa,wengine twafanywa nzi,
Twazaliwa na kukua,pasi malezi na mapenzi,
Ameshajilimbikizia, fisadi hawezi shindwa.

Ni wao na familia zao wanazozienzi,
Ni kisiwa wamekua, wengine kwa ushuzi,
Wanataka kujilia,bila yoyote maudhi,
Ameshajilimbikizia, fisadi hawezi shindwa.

Haki hujakupotea, dhuluma kuwa azizi,
Mali watajajimegea, makwao washehenezi,
Wengi wakawa wakiwa, watu wasio na radhi,
Ameshajilimbikizia, fisadi hawezi shindwa.

Tamaa hujapotea, kwa baadhi na baadhi,
Kura wakaikataa, na kuiona upuuzi,
Kujiandikisha pia, wasuse chao kizazi,
Ameshajilimbikizia, fisadi hawezi shindwa.

Uchu ukishavamia, siasa huwa na ganzi,
Watu huona udhia, kura kujawapa wezi,
Mwishowe hujaamua, kuyafanya mapinduzi,
Ameshajilimbikizia, fisadi hawezi shindwa.

Kinachofuatia, redio wani huwa wazi,
Na kitakachoendelea, hakitakuwa kwetu wazi,
Kusaga meno na kulia, yatakuwa maamkuzi,
Ameshajilimbikizia, fisadi hawezi shindwa.

Dawa acha kutumiwa, acha riziki za wizi,
Wacha mungu kuchagua, haki yawe maamuzi,
Na nchi kuendelea, wapeni wachapa kazi,
Ameshajilimbikizia, fisadi hawezi shindwa.

No comments: