Thursday, October 20, 2011

Nabii wajisimika

Nabii leo wazuka, wenyewe wajisimika,
Muumba wamemkwepa,wamejipa madaraka,
Sijui akikasirika, ni wapi watamwepuka,
Nabii wajisimika, Mungu-mtu sasa aja!

Magazeti yaandika, redio zinasikika,
Televisheni kuzuka, ndio zinathaminika,
Ndio waliookoka, nao kwao utaokoka,
Nabii wajisimika, Mungu-mtu sasa aja!

Nasikia kwa hakika, waliotokota hufika,
Na hawa wanaosifika, wapo wanaokujashuka,
Hupati unalotaka, hupewa utakaloshika,
Nabii wajisimika, Mungu-mtu sasa aja!

Miujiza watajika, mengine hutia shaka,
Sarakasi ukifika, utadhani yafanyika,
Dunia hii kufufuka, sijui wanakotoka,
Nabii wajisimika, Mungu-mtu sasa aja!

Maisha yakichemka, manabii hujazuka,
Wa namna hii hakika, wakati wao wafika,
Na ukiwa mshirika,huenda yakakufika,
Nabii wajisimika, Mungu-mtu sasa aja!

Nchi hii Tanganyika, sio kwanza wanazuka,
Waja, kisha kutoweka, vizazi husahaulika,
Maisha kuteremka,rahisi si kupandika,
Nabii wajisimika, Mungu-mtu sasa aja!

Umetaka hukutaka, wakija wanaozuka,
Ukipenda utaanguka, usipopenda utashuka,
Akili za Kiafrika, kaeni mzipe mwafaka,
Nabii wajisimika, Mungu-mtu sasa aja!

No comments: