Saturday, October 1, 2011

Utajafika wakati, viranja kutemwa mate!

Wakati utajafika, viranja kutemwa mate,
Wazidi kutoaminika, wasiwe chochote, lolote,
Wakawa watajirika, na yeyote wasimvute,
Utajafika wakati, viranja kutemwa mate!

Watu wasiponufaika, na kila pembe wadate,
Uongozi utanuka, na tena wasimeremete,
Na moto wataukoka, na humo wateketee,
Utajafika wakati, viranja kutemwa mate!

Wakubwa hawatabebeka, yaja shughuli tete,
Hakuna wa kusadikika, katika milki yote,
Manabii wakizuka, hata mbawa ziwaote,
Utajafika wakati, viranja kutemwa mate!

Atachoka Mwafrika,ndoto mbaya aziote,
Jua litababaika, lisambae anga lote,
Mwezi hautazunguka, giza liwe kotekote,
Utajafika wakati, viranja kutemwa mate!

Wa juu watajashuka, watembee na viwete,
Wale wanaosifika, ndoto za kutisha waote,
Nchi haitakalika,na nje wasiwaite,
Utajafika wakati, viranja kutemwa mate!

Ahadi zinapozikwa, matuta kote yaote,
Uvumilivu hushuka, tamaa watu wakate,
Mbele hakutaendeka,na kwenda nyuma wasite,
Utajafika wakati, viranja kutemwa mate!

Wakuu watababaika, usingizi waufute,
Alfajiri kudamka, na wasiende kokote,
Baragumu litasikika,wapigaji wawasute,
Utajafika wakati, viranja kutemwa mate!

Yatatemwa madaraka, na viongozi wagote,
Dhima iwe patashika, tena vuta nikuvute,
Malaika hawatashuka, na msaada wasiupate,
Utajafika wakati, viranja kutemwa mate!

Watagura vibaraka, bangi zao wazikoke,
Shari waliochagulika, hadharani ziwaoke,
Mashahidi kuandika, lisiponyoke lolote,
Utajafika wakati, viranja kutemwa mate!

No comments: