Sunday, October 23, 2011

Mafisadi waoanapo

Waoanapo mafisadi, mwananchi sema hapana,
Wa siasa mafisadi na wa dini kuoana,
Ni ndoa ya kuritadi, yafaa kuepukana,
Mafisadi wa siasa, waoapo wa kidini!

Taifa watalinadi, bei wakishapatana,
Mwananchi kuwa zawadi, ya wao wa nje mabwana,
Si uvumba wala uodi,uoza utaepukana,
Mafisadi wa siasa, waoapo wa kidini!

Watahurumiana kodi, maendeleo kubana,
Waje ndani bila hodi, watugeuze watwana,
Imani kuwa kuwadi, na kufa iwe kufaana,
Mafisadi wa siasa, waoapo wa kidini!

Watafanza kujinadi, michango kuchangiana,
Na sisi hatuna budi, na wao kuja achana,
Haijawa yetu jadi, madhambi kuchangiana,
Mafisadi wa siasa, waoapo wa kidini!

Tuiogopeni radi, ya Ahadi Maulana,
Hawapendi wakaidi, wajifanyao mabwana,
Hatuna budi turudi, kwake tukawa watwana,
Mafisadi wa siasa, waoapo wa kidini!

Ujibari na hasadi, kazilani Rahmana,
Ajua hao kuwarudi, kwa moto wenye laana,
Ikiwa hapana budi, duniani huwakana,
Mafisadi wa siasa, waoapo wa kidini!

Haoni haya fisadi, kaziye kusema sana,
Aghali akijinadi, aonekane muungwana,
Kumbe uoza ni jadi, na kwa mzazi ana laana,
Mafisadi wa siasa, waoapo wa kidini!

Tuepushe na kuwadi, Yaa annafi yaa rabana,
Dini zikawa abadi, huru na kwako za maana,
Kukuabudu tuhidi, na sio wengine bwana,
Mafisadi wa siasa, waoapo wa kidini!

No comments: