Sunday, October 23, 2011

'Taka niwe kama baba

Dekeza, dekeza baa, na rahisi kupotea,
Njiani mwana alilia, pipi wamnunulia,
Alilia motokaa, ya watu utanunua?
'Taka niwe kama baba, ndiko wanakoanzia!

Halahala msojua, kigeugeu dunia,
Chako bora ukijua, cha wengine kufubaa,
Visa watakufanyia, harabu lazima kua,
'Taka niwe kama baba, ndiko wanakoanzia!

Bahati wanaopewa, akili ya kuzaliwa,
Maisha hupigania, nafasi kujipatia,
Hawana wa kutegemea, na Mungu huwasaidia,
'Taka niwe kama baba, ndiko wanakoanzia!

Wamezuka Tanzania, wadekezaji twajua,
Nchi watuharibia, kwa mizoga kuchukua,
Huku wanajivunia,na wao eti wamezaa,
'Taka niwe kama baba, ndiko wanakoanzia!

Kazi zao kujisifia, na ushindani kujitia,
Nyimbo watakuimbia, kama wa kwetu mkiwa,
Kaingia Romania, katokea Italia,
'Taka niwe kama baba, ndiko wanakoanzia!

Na London kapitia, ili mpate kujua,
Hayo vipi yatusaidia, vijijini twajifia,
Na mahekalu wazua, shida zinakoelea,
'Taka niwe kama baba, ndiko wanakoanzia!

Watu wanawahadaa, ukata kushikilia,
Eti wamechaguliwa, wao hawakuteuliwa,
Utajiri ni balaa, masikini waambiwa,
'Taka niwe kama baba, ndiko wanakoanzia!

Maskini waelea, bahari ya ushujaa,
Matajiri na visiwa, vyenye ulinzi na taa,
Fukara hana mshumaa, kwa vijinga huungua,
'Taka niwe kama baba, ndiko wanakoanzia!

Kuendelea balaa, nisije kujiumbua,
Uongo sikuzoea, na ukweli mwakataa,
Uchi mnasema kavaa, sasa nini nitawaambia?
'Taka niwe kama baba, ndiko wanakoanzia!

Hawafunzwi utadhania, kazi nyingine kujua,
Kama nyani wanakaa,ya baba kuingojea,
Nani asiyechukia,kwenye nchi yenye njaa?
'Taka niwe kama baba, ndiko wanakoanzia!

No comments: