Monday, October 24, 2011

Nyumbani kwako mwenyewe

PAKA kama sio mwewe, nilivyokujadhania,
Kumbe mwenye nyumba wewe, ufanyayo nashangaa,
Ugonjwa au kiwewe, kichwani umeingia?
Nyumbani kwako mwenyewe, wawa kama paka mwizi?

Ni vipi ufikiriwe, na wanaokuangalia,
Mtu gani kama wewe, haijawahi tokea,
Ni yepi maruweruwe, akilini yameingia?
Nyumbani kwako mwenyewe, wawa kama paka mwizi?

Ni lazima uvizie, ndipo unapoingia,
Shurti uogopewe, na wote wanaokujua,
Watakudhania wewe, mwanga umekwishakua,
Nyumbani kwako mwenyewe, wawa kama paka mwizi?

Huna ufanyalo wewe, nanio anayeumia,
Ujinga ufanye wewe, lawama unaziktaa,
Ni nani akujali wewe,jambo usiosaidia,
Nyumbani kwako mwenyewe, wawa kama paka mwizi?

Tafuta radhi ya mamawe, usijifanye wajua,
Leo hii kamwangukie, na Mola atakusikia,
Sali na ukuchwe wee, bure havitakusaidia,
Nyumbani kwako mwenyewe, wawa kama paka mwizi?

Wamdharau mumewe, furaha utaijua?
Hajui wajua wewe, wazidi mharibia?
Nafasi upewe wewe, huna unalozingatia?
Nyumbani kwako mwenyewe, wawa kama paka mwizi?

Bora wenyewe wachukuwe, kidunchu kikabakia,
Nongwa kukukabidhi wewe, nje unayeangalia,
Nyumbani kwako mwenyewe, huwezi paangalia!~
Nyumbani kwako mwenyewe, wawa kama paka mwizi?

No comments: