Thursday, October 20, 2011

Mjivuni

Njia yake haikwepi, hayo yake majaliwa,
Kama refu au fupi, lazima kufuatilia,
Aendako kama kupi, yeye mwenyewe ajua,
Mjivuni njia fupi, na huona kaonewa.

Mbegu hugeuka kapi, kwa anachojivunia,
Maisha yake mafupi, binadamu hajajua,
Hata kama haogopi, hushtuka kulijua,
Mjivuni njia fupi, na huona kaonewa.

Kikusikitishacho kipi, laiti ungenambia,
Ningekupatia pipi, mpenzi uache kulia,
Haijapo hunenepi, sharti utafurahia,
Mjivuni njia fupi, na huona kaonewa.

Huruma yangu upapi, mengi nimevumilia,
Bado wajifanya chupi, lazima kujavuliwa,
Uendako huko kupi, umeshindwa kuyajua,
Mjivuni njia fupi, na huona kaonewa.

Walishashindwa wangapi, wewe unang'ang'ania,
Kikukondeshacho kipi, kama si ya kujitakia,
Furaha yako iwapi, nje ukiifuatilia?
Mjivuni njia fupi, na huona kaonewa.

Nimekuonea lipi, kama si kujitakia,
Mimi na wewe wapi, tulipokujakosania?
Nimekutenda mangapi, na haukunisaidia?
Mjivuni njia fupi, na huona kaonewa.

Kiburi sawa na nepi, mtu mzima kuvaa,
Nikufungue kwa vipi, macho ujue dunia?
Unakokwenda ni kupi, kusikokujajutia?
Mjivuni njia fupi, na huona kaonewa.

No comments: