Thursday, October 20, 2011

Mambo yakishakushinda

Mlango kama si wazi, usifosi kuingia,
Kuna mingine iwazi, jaribisha kupitia,
Kuelewa hili kazi, subira sio tabia,
Mambo yakishakushinda, acha, kubali yaishe!

Usije ichuna ngozi, na mkono kuumia,
Usishikwe kikohozi, kwa hodi kung'ang'ania,
Umefungwa hauwezi, kwingine sasa pitia,
Mambo yakishakushinda, acha, kubali yaishe!

Kibaya king'ang'anizi, riziki huja potea,
Unakuwa ni dumizi, pale pale kulilia,
Hayasaidii machozi, mlango hayotofungua,
Mambo yakishakushinda, acha, kubali yaishe!

Vipindi ni angalizi, na nadra kutimia,
Ikiwa hauyawezi, yanini kujagombea,
Kiinimacho mbalamwezi, hajui asiyeyajua,
Mambo yakishakushinda, acha, kubali yaishe!

Usimngoje mtenzi, jambo kuja kukutendea,
Na usiipande ngazi, kushuka unapotakiwa,
Kitumbua si andazi, ashakum ni staha,
Mambo yakishakushinda, acha, kubali yaishe!

Mvua za kiangazi, sio za matumaini,
Wapo wa nyumba wajenzi, vigumu kuishi ndani,
Moyo nauacha wazi, anabaini Matini,
Mambo yakishakushinda, acha, kubali yaishe!

Shairi nimedarizi, hekima kuibaini,
Natumai uongozi, watoka kwako Bathini,
Nipandishe hii ngazi, nikakae ghorofani,
Mambo yakishakushinda, acha, kubali yaishe!

No comments: