Saturday, October 29, 2011

Hamsini yanihini

Afkani siamini, hamsini majinuni,
Sijailola nishani, na medali sizioni,
Tasnia hii gani, hamsini yanihini,
Yanihini hamsini,naishindwa tathmini.

Tata nilishabaini, ugumu sikamini,
Ni likubwa letu deni, kuliko pato yakini,
Na pengine hazinani, thamani yake majani,
Yanihini hamsini,naishindwa tathmini.

Ni Kaleb na Kaini, wananchi na wahisani,
Na viongozi nchini, wengine mabaniani,
Na kiatu yumkini, ni dawa ila siioni,
Yanihini hamsini,naishindwa tathmini.

Nilichokifanya ni nini, sijajua kwa yakini,
Nilishindwa kitu gani,hadi bado maskini,
Ujinga na uzaini, wachangia ktiu gani ?
Yanihini hamsini,naishindwa tathmini.

Nimefanyiwa na nani, nami nimefanyiwani,
Kwa shilingi na pauni, nimepata kitu gani,
Ni asilimia gani, yangu na hao wageni,
Yanihini hamsini,naishindwa tathmini.

Wamekwiba kitu gani, tangia ya ukoloni,
Na leo niko taabani, waendelea kufanyani,
Isiwe hesabu za nyani, daima nusu shakani,
Yanihini hamsini,naishindwa tathmini.

Au biashara guni, gumba isiyo auni,
Wanunua hamsini, wauza kwa ishirini,
Au mtaji wa deni, kwa riba uhasarani,
Yanihini hamsini,naishindwa tathmini.

Hainingii akilini, mimi kuwa shereheni,
Ni ndoa ya majinuni, hajui ya kesho ni nini?
Atumia milioni, kesho aomba thumuni,
Yanihini hamsini,naishindwa tathmini.

Walopata wamewini, muwachache furahini,
Na ndivyo ya duniani, yanavyokuwa vichwani,
Kwani miye kitu gani, apataye mwanandani,
Yanihini hamsini,naishindwa tathmini.

Kitendawili yakini, kwa walio mashakani,
Na mgumu mtihani, kwa wasio majinuni,
Kombakomba wako mjini, kukavu kwetu shambani,
Yanihini hamsini,naishindwa tathmini.

Maji hatunywi bombani, tunakunywa topeni,
Matofali niamini, ndio viti mashuleni,
Kompyuta hatuioni, twaisikia redioani,
Yanihini hamsini,naishindwa tathmini.

Vijiji ni nchi gani, nina mashaka kichwani,
Si Tanzania nadhani, lazima sayari ngeni,
Kama hamuamini, wakubwa tembeleeni,
Yanihini hamsini,naishindwa tathmini.

Hizo taa za mjini, zisiondoe uoni,
Nchi bado maskini, na watu wako taabani,
Sherehe tuziageni, tufanye ya afueni,
Yanihini hamsini,naishindwa tathmini.

No comments: