Sunday, October 9, 2011

Rais au raia?

Hivi mwenye nchi nani, rais au raia,
Hili sio yumkini, wananchi twapinduliwa,
Tunaoweka kazini, ubwana wanachukua,
Rais au raia, kati yao nani bosi?

Kati yao bosi nani, rais au rais,
Afrika mashakani, wote hili tunajua,
Mtu ukishamthamini, dharau anaingia,
Rais au raia, kati yao nani bosi?

Tumegeuzwa manyani, nje wanatushangaa,
Uoga wetu wa nini, nafasi kuichukua,
Iweje mtu ofisini, mwenye mali kujitia?
Rais au raia, kati yao nani bosi?

Hazina huwa shakani, fisadi wakiingia,
Mbawa noti hubaini, kwa watu zikaishia,
Na raia masikini, maneno waambulia,
Rais au raia, kati yao nani bosi?

Ubinafsishaji baini, kitanzi wametutia,
Mashirika hatuoni, na fedha zimepotea,
Hakika hawa wahuni, siogopi kuwaambia,
Rais au raia, kati yao nani bosi?

Uchangiaji nchini, jahazi lazidi waa,
Hatuoni kwa yakini, kitu tulichofanyiwa,
IMF wadaini, mtegoni kututia,
Rais au raia, kati yao nani bosi?

Viongozi mikoani, sio wa kuwachagua,
Tunafanya ya utani, rais kuwateua,
Tutapata watu gani, mikoa kuendelea?
Rais au raia, kati yao nani bosi?

Nchi yataka anwani, visheni au ruia,
Hivi leo twazaini, kwa mbwembwe na sanaa,
Hii jama nchi gani, iendako isojua?
Rais au raia, kati yao nani bosi?

Ni watu wa mjini, umeme wanaolilia,
Huko kwetu vijijini, giza tumeshalizoea,
Na miaka hamsini, kwetu ni kama milenia,
Rais au raia, kati yao nani bosi?

Hivi twajivuna nini, watu wetu kuwafanzia,
Mimi naona utani, tena mkubwa mzaha,
Akili ninaamini, sasa tungelitubia,
Rais au raia, kati yao nani bosi?

Tumekwaza vijijini, na malengo kupotea,
Ni heri ya mkoloni, kwa hulka na tabia,
Ni bure tunajithamini, bila watu kuangalia,
Rais au raia, kati yao nani bosi?

Nistahi ya Manani, kwa ulimi na nasaha,
Nimeshakiri moyoni, uongo nitakimbia,
Marufuku uzaini, kwangu kuukurubia,
Rais au raia, kati yao nani bosi?

Najenga yangu medani, sifuati ya dunia,
Ila naomba yamini, kwa shahada na dua,
Wabaya ukibaini, wewe utamalizia,
Rais au raia, kati yao nani bosi?

Watu wangu wathamini, na juu kuwanyanyua,
Ittunze yao amani, na umoja kuringia,
Ila watie shakani, wote wanaowahadaam
Rais au raia, kati yao nani bosi?

Na leo hapa nchini, katiba twazungumzia,
Anastahili nani, mchakato kuamua?
Raia ninaamini, haki zote wanazoa,
Rais au raia, kati yao nani bosi?

Jishusheni chini jamani, kazi kutuachia,
Msiogope uhuni, wallahi hatutawafanzia,
Kuchinja kwetu amini, kunyonga hatukuzoea,
Rais au raia, kati yao nani bosi?

Tuepuke na udini, waumini kuhadaa,
Mtatutia usononi, nchi ikaja pagawa,
Oneni haya jamani, uozo kutuachia,
Rais au raia, kati yao nani bosi?

Wito huu sikieni, na nyie wanasheria,
Juzuu mzibaini, ukweli kuwaambia,
Msikae utumwani, shari haitachagua,
Rais au raia, kati yao nani bosi?

Malenga nawaombeni, kizazi kuangalia,
Njia yao iwe laini, kesho watakakopitia,
Nafsi zenu dhibitini, urithi kujawaachia,
Rais au raia, kati yao nani bosi?

No comments: