Thursday, October 20, 2011

Milioni hamsini

Ninahoji maamuzi, siasa sizibaini,
Twakosaje viongozi, na sisi mamilioni,
Wananiambia wajuzi, milioni hamsini,
Twakosaje viongozi, milioni hamsini?

Naona kuna ajizi, sababu mimi sioni,
Kuchagua sio kazi, penye siasa makini,
Pasipo na kura wizi, na haki tukithamini,
Twakosaje viongozi, milioni hamsini?

Njaa ni yetu maradhi, yazidisha umaskini,
Tunachagua viazi, watu hatuwathamini,
Tunaokota nazi, akili zisizobaini,
Twakosaje viongozi, milioni hamsini?

Au pengine Azizi, katuona maaluni,
Katuachia kizazi, kupata waso makini,
Ife miji na kamazi, hadi warithi wageni,
Twakosaje viongozi, milioni hamsini?

Sijapata ufumbuzi, najiona majinuni,
Wakulima na wakwezi, kuongozwa na wahuni,
Mliwapatiaje kazi, watu wasiowathamini?
Twakosaje viongozi, milioni hamsini?

Zimezagaa mbaazi, shambani pia njiani,
Huokota mabazazi, mashuzi nani atamani,
Kweli hapana wajenzi,miti iliposakini,
Twakosaje viongozi, milioni hamsini?

Tumkurubie Hafizi, ambaye wetu Manani,
Atufanyie majazi, wepesi wa mitihani,
Nchi yataka ujenzi, kuondoa umaskini,
Twakosaje viongozi, milioni hamsini?

Nchi yataka ujenzi, kuondoa umaskini,
Atupe wake ujuzi, tuweze kuwa makini,
Tupatilize washenzi, na wafanyao utani,
Twakosaje viongozi, milioni hamsini?

Ah, Yaghaniyu, Ya Mani, sitatul tuiimaizi,
Tusijikwae njiani, twataka bora makazi,
Firdausi kwetu shani, ustadhi na wanafunzi,
Twakosaje viongozi, milioni hamsini?

No comments: