Wednesday, October 19, 2011

Ustawi wa Jamii

Ustawi wa jamii, wallahi kama yatima,
Mie ninatoa rai, tufanyavyo sio vyema,
Kama hatufikirii, basi si watu wazima,
Ustawi wa Jamii, unahitaji wizara.



Fukara idara hii, siku zote iko nyuma,
Hupachikwa kwa nanihii, na hii ni kubwa dhuluma,
Sasa tumeyakinai, twataka wizara nzima,
Ustawi wa Jamii, unahitaji wizara.


Ni kubwa sana jamii, hili lataka hekima,
Jambo la kutanabahi, muhimu kuipa dhima,
Iweze kutustahi, kwa nyenzo pia huruma,
Ustawi wa Jamii, unahitaji wizara.

Wazee twaitumai, kuzipunguza dhuluma,
Endapo tukiwa hai, tusiwe zigo kwa umma,
Uzeeni kutustahi, tufe na yetu heshima,
Ustawi wa Jamii, unahitaji wizara.

Jamii haifurahi, kuteseka kwa vilema,
Majina ni usanii, tutakalo yenye hima,
Kuwanyaapa nishai, hawa ni wana wa umma,
Ustawi wa Jamii, unahitaji wizara.

Wakithiri majeruhi, waso baba au mama,
Twawanadi kisanii, majina ya takrima,
Watoto wa mitaani, huku bado wanakwama,
Ustawi wa Jamii, unahitaji wizara.

Wajane nao wadai, tutunze yao heshima,
Wizara iwastahi,tusiache ya karama,
Nao wapate furahi, kwa kutunzwa nao umma,
Ustawi wa Jamii, unahitaji wizara.

Masikini wazirai, kwa dhiki, njaa na homa,
Ustawi wa jamii, hawaoni wake wema,
Mchango wanaudai, serikali fanya hima,
Ustawi wa Jamii, unahitaji wizara.

Watoto watundu nai, kote wanavyorindima,
Jela zao hazifai, zinazo nyingi tuhuma,
Kuwaokoa sijui, kama tunayo neema,
Ustawi wa Jamii, unahitaji wizara.

Vijana hatuwatumii, JKT wanasema,
Waweza faa jamii, nao kujifunza dhima,
Ajira wazisabahi, kila wakifanya vyema,
Ustawi wa Jamii, unahitaji wizara.

Afya shughuli hii, iwe peke yasimama,
Upacha hautufai, upande unaegema,
Rais pokea rai, kwa heshima na taadhima,
Ustawi wa Jamii, unahitaji wizara.

No comments: