Sunday, October 23, 2011

Sauti itasikika

Hadi ng'ambo kaburini, sauti itajafika,
Sauti hawatahini, leo wanaosifika,
Utazimika ubani, na marashi kutoweka,
Sauti itasikika, hadi ng'ambo kaburini.

Haki wanaoamini, ni watu wa kuteseka,
Ila kilicho moyoni, daima huwapeleka,
Binadamu si Manani, hilo wana uhakika,
Sauti itasikika, hadi ng'ambo kaburini.

Huwajua wazaini, na yanayokujakuwafika,
Ukweli walishabaini, si rahisi kutumika,
Mkataba huughani, hakuna vuka mipaka,
Sauti itasikika, hadi ng'ambo kaburini.

Wababe wanaodhani, waweza kunyamazika,
Hukuta ni mtihani, usiowezekanika,
Kufaulu hubaini, kwao huwa ni mashaka,
Sauti itasikika, hadi ng'ambo kaburini.

Waondoke duniani, bado sauti hufika,
Mizuka na maruhani, vuguvugu hulidaka,
Wakawa ni mashakani, hadi kifo kuwafika,
Sauti itasikika, hadi ng'ambo kaburini.

Hili ninaliamini, watazame wahusika,
Kusi hadi kaskazini hapa kwetu Afrika,
Viongozi mashetani, Mola anawamulika,
Sauti itasikika, hadi ng'ambo kaburini.

Si watu wa kuamini, vyeo kwao huabudika,
Ni vipofu duniani, moto wao wanapika,
Sio bora, watu duni,watakujabainika,
Sauti itasikika, hadi ng'ambo kaburini.

Isiwe yako idhini, wangu Rahimu Rabuka,
Kuniweka duniani, dhuluma ikafanyika,
Niepushe mitihani, nisije kudanganyika,
Sauti itasikika, hadi ng'ambo kaburini.

No comments: