Tuesday, October 18, 2011

Uongozi si mgumu

Uongozi sio kazi, kama watu wasikia,
Na si mkubwa ujuzi, kama watu wafwatia,
Hii tarafu azizi, na watu huwasaidia,
Uongozi si mgumu, watu hawaongozeki!

Binadamu sio mbuzi, ila wakitaka huwa,
Ikawa kwako ni kazi, walipo kuwanyanyua,
Wakakuachia mashuzi, na uchafu uliojaa,
Uongozi si mgumu, watu hawaongozeki!

Ardhi pia makazi, wala hazina ghasia,
Mashine kwa mautmizi, kila kitu huridhia,
Fedha haina maudhi, kwa vyovyote huitumia,
Uongozi si mgumu, watu hawaongozeki!

Pale palipo na kazi, ni binadamu kumvaa,
Hata awe na ujuzi, bado hukuharibia,
Ajira huwa ajizi, wakazua na balaa,
Uongozi si mgumu, watu hawaongozeki!

Fadhila mwoneshe mbuzi, waswahili wakwambia,
Binadamu ni maudhi, hili kweli zingatia,
Bora kapu la viazi, haliwezi kusumbua,
Uongozi si mgumu, watu hawaongozeki!

Uongozi si matanuzi, watu watakuchukia,
Jamali za majahazi, shehena kuzichukua,
Kutumika faradhi, na suna ni kutumia,
Uongozi si mgumu, watu hawaongozeki!

Uongozi ni uzazi, kuzaa yaliyo mapya,
Wataka mengi uzuzi, watu wakafuatilia,
Maisha ni uvumbuzi, si ofisini kukaa,
Uongozi si mgumu, watu hawaongozeki!

Uongozi ni malezi, wa chini ukawalea,
Wapande za juu ngazi, na urithi kuchukua,
Mzee asiyemaizi, hili atalizuia,
Uongozi si mgumu, watu hawaongozeki!

No comments: