Tuesday, October 11, 2011

Wapenda watu wachache

Wachache watu wapenda, watu ukubwa wataka,
Kila mtaka kupanda, si bure hushughulika,
Kuna linalomdunda, anataka kulishika,
Wapenda watu wachache, wapenda ukubwa wengi!

Ya kwake yanamshinda, ya wengine atawika?
Na jamii ya kuvunda, harufu haitotoweka,
Ndio kote walotanda, kipya hakitashuka,
Wapenda watu wachache, wapenda ukubwa wengi!

Wateremka udenda, kwa ukata kufutika,
Au kujenga kiwanda, kwa fedha ya washirika,
Au shirika kuunda, kufilisi walochoka,
Wapenda watu wachache, wapenda ukubwa wengi!

Wengine wamevurunda, hakuna lililoitika,
Wataka chuma matunda, kwa wizi wa kuaminika,
Katika hilo huwatenda, hakuna mbwa kubweka,
Wapenda watu wachache, wapenda ukubwa wengi!

Viongozi kama nunda, mali hulimbikizika,
Ni Jetta wanajipenda, na hawana mshirika,
Na kwao kama kdonda, ni ndugu hadi kuzika,
Wapenda watu wachache, wapenda ukubwa wengi!

Akili zao huganda, kwa ukubwa kuutaka,
Sifa wanavyozipenda, ndarahima hutumika,
Huwa radhi kula ganda, ilimradi kukubalika,
Wapenda watu wachache, wapenda ukubwa wengi!

Wanapokosa hukonda, nyumbani hakutokalika,
Na akiwa mziwanda,kitindamimba hutaka,
Maajabu mwenye kenda,moja kwa nguvu kutaka,
Wapenda watu wachache, wapenda ukubwa wengi!

Hawa watu wamepinda, vigumu kueleweka,
Hutaka kunywa mafunda,ilhali wanabweka,
Mbwa hawezi kutenda,yale wanayoyataka,
Wapenda watu wachache, wapenda ukubwa wengi!

Waliliazo ni honda, za mchina nani ataka?
Hudai punda kupanda, sisi miguu imekatika,
Mahekalu huyaunda, sisi twashindwa ezeka,
Wapenda watu wachache, wapenda ukubwa wengi!

Ghorofa wanazipanda, sisi ngazi tunashuka,
Hata kama twawapenda, vipi mkono kuwashika?
Na katika yao ajenda,hili halijasomeka,
Wapenda watu wachache, wapenda ukubwa wengi!

Wasanii wa kuwanda, mitaani wakifika,
Huku na huku huranda, na mikono kuwashika,
Vitoto vilivyobwanda, mikononi kuvishika,
Wapenda watu wachache, wapenda ukubwa wengi!

Nyoyo zinavyowadunda, si dhiki kueleweka,
Kubwa wataka mkanda, televisheni kuweka,
Waonwe wanawapenda, wasiowapenda hakika,
Wapenda watu wachache, wapenda ukubwa wengi!

Najenga changu kibanda, mchanga ninautaka,
Na mbele siwezi kwenda, bado daraja kuvuka,
Miguu imeniganda, naenda kupumzika,
Wapenda watu wachache, wapenda ukubwa wengi!

No comments: