Tuesday, October 18, 2011

Wapaswa kumdharau, auzaye kura yake.

AUZAYE kura yake, wapaswa umdharau,
Anajali tumbo lake, maisha anadharau,
Muache abaki pweke, huyo mtu wa kusahau,
Wapaswa kumdharau, auzaye kura yake.

Udugu usimshike, huyo sawa na mafuu,
Ili usalimike, umwepuke ni bahau,
Ni muhali mambo yake, kufanikiwa falau,
Wapaswa kumdharau, auzaye kura yake.

Daima pembeni mweke, hana kichwani juzuu,
Vigumu aneemeke,utumwa wake tambuu,
Acha jiwe aeleke, huyu ana makuruhu,
Wapaswa kumdharau, auzaye kura yake.

Demokrasi makeke, na miguu huwa juu,
Kichwa chini kizamike, na kipya huwa kikuu,
Zawadu yake mateke, mchuuzi kura yake,
Wapaswa kumdharau, auzaye kura yake.


Uweledi tuutake, kwa misemo na nahau,
Avujaye tumwezeke, sio mtu wa kunukuu,
Kisimamacho kianguke,kilo chini kije juu,
Wapaswa kumdharau, auzaye kura yake.

Historia ina upweke, maana ni kuukuu,
Uzee kama mvuke,si wa chini waenda juu,
Sio yote tuwacheke, mengine dawa nafuu,
Wapaswa kumdharau, auzaye kura yake.

Tuendako kuendeke, nguvu tutazisahau,
Tujengacho kijengeke, teknolojia tukubuhu,
Ili nasi tutajirike,tusijiuze bei nafuu,
Wapaswa kumdharau, auzaye kura yake.

No comments: