Thursday, October 20, 2011

Uzuri na Ubaya

HALI ya hewa yacheza, binadamu aicheza,
Shere anaifanyiza, ya mbele bado kuwaza,
Mwenyewe ajidumaza, adhani yeye akwazwa,
Uzuri wajitembeza, ubaya unajiuza.

Dunia twaigeuza, wazuri wajitembeza,
Hali wabaya wajiuza, ninabaki kuuliza,
Haya tukishamaliza, ni mangapi twabakiza?
Uzuri wajitembeza, ubaya unajiuza.

Thamani umechuuza, uzuri wajitembeza,
Kila mtu wamtatiza, japo mate ayameza,
Gharama hatoiweza, na mchuuzi huchuuzwa,
Uzuri wajitembeza, ubaya unajiuza.

Kibaya kinajiuza, dunia ya miujiza,
Na bei hujiongeza, kila kinakopitiza,
Wanunuzi wakimbiza, kupata hawajaweza,
Uzuri wajitembeza, ubaya unajiuza.

Uzuri wabembeleza, na watu wanauiza,
Baba anatukataza, na mama anaapiza,
Shangazi naye abeza, mjomba anagombeza,
Uzuri wajitembeza, ubaya unajiuza.

Uzuri umejichakaza, thamani umeipoeza,
Nuru imekuwa giza, imebaki kuomboleza,
Maradhi ukiingiza, huna utakachobakiza,
Uzuri wajitembeza, ubaya unajiuza.

Dunia yatuduwaza, kizuri kujitembeza,
Ni nani wameukwaza, chini sasa wajiburuza,
Na swali, je, unaweza, kuja tena kujiuza?
Uzuri wajitembeza, ubaya unajiuza.

Sala inayopendeza, Mushawari kuhimiza,
Ajua kutengeneza, aali visivyojitembeza,
Naye ukimbembeleza,atakujazia chaza,
Uzuri wajitembeza, ubaya unajiuza.

Kazi nimeimaliza, malenga nawaagiza,
Fanyeni kupeleleza, siri hii kuchunguza,
Huu mkubwa muujiza, haufai kupuuza,
Uzuri wajitembeza, ubaya unajiuza.

No comments: