Monday, October 3, 2011

Mbunge mtetea chama

Mbunge mtetea chama, si mbunge wa raia,
Mdomo akiachama, aweza kuwashindilia,
Tumbo lake likisoma, hatajua yako njaa,
Mbunge mtetea chama, si mbunge wa wananchi!

Toka mwanzo utamsoma, vifurushi akigawa,
Krediti huazima, kulipwa akitarajia,
Hukufanya muadhama, kura yako akingojea,
Mbunge mtetea chama, si mbunge wa wananchi!

Unaweza kumpima, huko alikotokea,
Meli nyingi zilizama, nahodha alipokuwa,
Leo eti chake chama, vinginevyo chatwambia,
Mbunge mtetea chama, si mbunge wa wananchi!

Hawa ni watu wa kalima, ya umimi wa kupaa,
Ni sume yenye heshima, maendeleo huua,
Zichunguzeni tuhuma, ukweli mtaujua,
Mbunge mtetea chama, si mbunge wa wananchi!

Maisha yao kiama, tayari kishaingia,
Na kaumu hujakwama, nyuma wakijamfuatia,
Vipi ovu kuwa jema, hata upya likizaliwa?
Mbunge mtetea chama, si mbunge wa wananchi!

Macho nani kufungua, akawa kwa hili mjuzi,
Watu kujaendelea, tunataka viongozi,
Tafiri na kuchambua,yenye hadhi maamuzi,
Mbunge mtetea chama, si mbunge wa wananchi!

Wananchi na wanachama, njaa kwetu ni kitanzi,
Wachache wanaojua, mumiani twawaenzi,
Wakijakufichuliwa, mmekwisha ni wa juzi,
Mbunge mtetea chama, si mbunge wa wananchi!

Kifo tunakikumbatia, Nungwi hadi Mlandizi,
Makaburi twachimbia, hali wa hai wakazi,
Msiba twashangilia, sherehe kwetu majonzi,
Mbunge mtetea chama, si mbunge wa wananchi!

Nguvu zimeniishia, niseme nini mzazi,
Nimebakia kulia, giza tunavyolienzi,
Laiti ningelijua, yaja kuwa ni majonzi,
Mbunge mtetea chama, si mbunge wa wananchi!

Serikali yatakiwa, kufanya ya kwake kazi,
Na wabunge nao pia, wana ya kwao faradhi,
Vipi moja kuja kuwa, bila kuzusha majonzi?
Mbunge mtetea chama, si mbunge wa wananchi!

Jalali nakwangukia, mfalme mwenye enzi,
Nchi yetu kujalia, waje wema viongozi,
Na salama kuja kuwa, kijacho hicho kizazi,
Mbunge mtetea chama, si mbunge wa wananchi!

No comments: