Saturday, October 29, 2011

Wazungu hawana kazi

Uzunguni kiangazi, hakuna wa kuajiri,
Maprofesa wazuzi, wanakuwa mafakiri,
Kisa si kukosa kazi, ila hapana mwajiri,
Wazungu hawana kazi, wangoja tuwaajiri!


Marekani kaskazi, wamekwisha waajiri,
Wanazuka mabitozi, kuugani ushairi,
Ngonjera za nguvu kazi, na ajira kutabiri,
Wazungu hawana kazi, wangoja tuwaajiri!

Mkowapi viongozi, wazungu kuwaajiri,
Nchi hamuiendelezi, na fursa kuabiri?
Hii neema ya Mwenyezi, nyie mwaiona shari?
Wazungu hawana kazi, wangoja tuwaajiri!

Tunataka wafanyakazi, tena walio hodari,
Kuendeleza ujenzi, barabara na bandari,
Kadhalika uvumbuzi, wa meli na manowari,
Wazungu hawana kazi, wangoja tuwaajiri!

Umeme kwetu ajizi, mitambo sio akheri,
Tuwaiteni wajuzi, kuja kufanya urari,
Sayansi kuipa kazi, kuepukana na shari,
Wazungu hawana kazi, wangoja tuwaajiri!

Wahandisi waso kazi, na waliokwishajiajiri,
Hili hamjalimaizi, kuwepo kwa askari,
Waliosoma na hadhi, na ufundi kukariri?
Wazungu hawana kazi, wangoja tuwaajiri!

Ubia mkimaizi, nchi itapata heri,
Ni mengi sana majenzi, sasa hatutaghairi,
Hata vijiji kuenzi, karne hii viabiri,
Wazungu hawana kazi, wangoja tuwaajiri!

Inanitia simanzi, kuona kuna jeuri,
Na pengine ni ushenzi, majivuno na kiburi,
Nchi yataka wajenzi, sisi twafanya hadhari,
Wazungu hawana kazi, wangoja tuwaajiri!

Amkeni viongozi, twataka unda magari,
Kununua kubwa kazi, tunazidi ufakiri,
Ama baadhi na baadhi, inkishafi sighairi,
Wazungu hawana kazi, wangoja tuwaajiri!

Kosa akili ya ujuzi, lakini sio minghairi,
Usikose utambuzi, pale palipo na heri,
Majuu kwenye wajuzi, kunataka itihari,
Wazungu hawana kazi, wangoja tuwaajiri!

Wahandisi wanafunzi, wazungu watahadhiri,
Wajifunze kwenye kazi, reli zote kuabiri,
Safari na uchuzi, uje kuwa wa kheri,
Wazungu hawana kazi, wangoja tuwaajiri!

Utafanyika ujenzi, Unguja binghairi,
Meli mpya zienzi, tuziondoe hatari,
Sisi tuwe ni wajenzi, na wauza kwa fahari,
Wazungu hawana kazi, wangoja tuwaajiri!

Yatafanyika majenzi, makubwa yaliyo kheri,
Nchi irindime kazi, bila kitu kusubiri,
Waongezeke wajuzi, na makubwa kubashiri,
Wazungu hawana kazi, wangoja tuwaajiri!

No comments: