Sunday, October 23, 2011

Napenda ishi kijijini

Maisha hapa mjini, hayana lililo jema,
Naishi kwa kubaini, vijiji vingali nyuma,
Mengi hayapatikani, mahitaji wanakwama,
Ningeishi kijijini, zingekuwepo huduma.

Ningehamia mwandani, na mi niende kulima,
Nikaishi vijijini, hewa isiyo tuhuma,
Ufugaji kubaini, kuku,bata wa hakika,
Ningeishi kijijini, zingekuwepo huduma.

Tena yaishe kinywani, mayai yenye mashaka,
Kienyeji kusaini, mkataba wa hakika,
Maradhi ningehaini, niishi pasi dhihaka,
Ningeishi kijijini, zingekuwepo huduma.

Matunda ningeyawini, shambani yakapandika,
NIkavuna kwa hisani, juisi kutengezeka,
Upepo wa bustani, unipe kupumzika,
Ningeishi kijijini, zingekuwepo huduma.

Ningeepuka uhuni, pikipiki kuepuka,
Bajaji kuacha tauni, kelele kutosikika,
Daladala za kihuni, nazo hazitosikika,
Ningeishi kijijini, zingekuwepo huduma.

Kawaambie madiwani, huduma wakiipeleka,
Maji yawe kijijini, mjini ninaondoka,
Sioni sababu gani, mjini kujateseka,
Ningeishi kijijini, zingekuwepo huduma.

Mbunge naye abaini, hapa ninalazimika,
Ninabakia mjini, umeme nami shirika,
Kazi zangu si auni, bilao hazitafanyika,
Ningeishi kijijini, zingekuwepo huduma.

Umeme wa kijijini, siku utakapowaka,
Nitaondoka mjini, niende kushereheka,
Pasiwe abautani, tena kwa mingi miaka,
Ningeishi kijijini, zingekuwepo huduma.

No comments: