Wednesday, October 19, 2011

Waandishi wa habari

Muamana hupotea, kama kufa na maisha,
Mwandishi akiolewa, na wakubwa wakumtisha,
Kazi yake hujifia, maiti ende kuosha,
Mwandishi akiolewa na wanasiasa kesha!


Rwanda kilichotokea, waandishi walizusha,
Njia mnayoelekea, huko mtakujatufikisha,
Halahala nawaambia, damu hamwezi iosha,
Mwandishi akiolewa na wanasiasa kesha!

Kila mtu ana njaa, wao sasa wazidisha,
Tumbo linawatumbukia, wana kifafa cha kuangusha,
Senti wakishapewa, waka'nga bila kuosha,
Mwandishi akiolewa na wanasiasa kesha!

Wahariri nahofia, hakuna wa kuwawajibisha,
Habari wanazitoa, mwandishi kaziegesha,
Upande zinalalia, akishapokea rushwa,
Mwandishi akiolewa na wanasiasa kesha!

Yanini unazitoa, na gazeti kuchapisha,
Kidole hukunyookea, na hili linasikitisha,
Inafaa kupakuliwa, upya mwende kuoshwa,
Mwandishi akiolewa na wanasiasa kesha!

Mauzo yanavyopungua, uongo ndio wazusha,
Uhuru wanaulilia, wa uongo kutupasha,
Jukumu mlilopewa, ndilo mnalotufundisha,
Mwandishi akiolewa na wanasiasa kesha!


Mwapika na kupakua, siasa za kupotosha,
Uchumi mnategemea, nani wa kuja unyoosha,
Kazi yenu mmekalia, umbeya na rasharasha,
Mwandishi akiolewa na wanasiasa kesha!

Juu nyie mwatakiwa, wanasiasa kuwapasha,
Wajibu kuwazindua, wasifanze ya kuchusha,
Nchi ipate endelea, kwenye dhiki kutuvusha,
Mwandishi akiolewa na wanasiasa kesha!

Wenye mali nawaambia, haya nyie mmezusha,
Wazee kuwaondoa, vijana mkawapandisha,
Busara imepotea, nyuzirumu zinaisha,
Mkiishanunuliwa, nani atatuwezesha,

Wazee wanatakiwa, ujinga kusimamisha,
Hekima wakaigawa, miiko kusimamisha,
Wale wanaochaguliwa, njaa kutowatingisha,
Mwandishi akiolewa na wanasiasa kesha!

Heshima najivunia, warithi wasikitisha,
Uzaini wahadaa, wafanya yanayochosha,
Nani wa kuwasaidia, kuyatakasa maisha,
Mwandishi akiolewa na wanasiasa kesha!

Mashehe nawausia, waandishi kuwapasha,
Dini yao kuijua, na moto kuwaepusha,
Dhamana yao ulua, dhambi nyingi kubebeshwa,
Mwandishi akiolewa na wanasiasa kesha!

Watakiwa kuongoa, na sio kufarakisha,
Watakiwa kushuhudia, na sio kujakanusha,
Wahesabiwa wadaiwa, umma wanapoupotosha,
Mwandishi akiolewa na wanasiasa kesha!

No comments: