Tuesday, October 11, 2011

Ghorofa kwenye kinyesi

Nchi hii nchi gani, ulaji na makamasi,
Maudhi hatuyaoni, na hatuna wasiwasi,
Twakaribisha wageni, mitaa ina kinyesi,
Ustaarabu gani wa ghorofa kwenye kinyesi?

Ni ustaarabu gani, nauliza kadamnasi,
Kinyaa hatukioni, utadhani ibilisi,
Twamuaibisha nani, kama si sisi watesi,
Ustaarabu gani wa ghorofa kwenye kinyesi?

Mvua tukibaini, twafungulia vinyesi,
Mitaa na uchochoroni, zinafurika nuksi,
Wengine ni muumini, hawawezi hii kasi,
Ustaarabu gani wa ghorofa kwenye kinyesi?

Zinavyoota mjini, kama uyoga fususi,
Ila mazingira duni, na hewa yake nyeusi,
Maofisa hawabuni, lolote la kuasisi,
Ustaarabu gani wa ghorofa kwenye kinyesi?

Dar es salaam jijini, utadhania chunusi,
Ni mengi utafichua, ukifanya udamisi,
Na kisha kuyagungua, ya uchache ufanisi,
Ustaarabu gani wa ghorofa kwenye kinyesi?

Ninakuwa mashakani, eti tuna jiniasi,
Ni goli li kimiani, au tonge la msosi,
Halitoingia ndani, koromeo litaasi,
Ustaarabu gani wa ghorofa kwenye kinyesi?

Naona uhayawani, tena mkubwa utusi,
Mbona hatuamshani, tukakijua kiasi,
Kamwe hatutoki ndani, bila kuvaa libasi,
Ustaarabu gani wa ghorofa kwenye kinyesi?

Chai ikiwa tumboni, nje waweza ifosi,
Unapokuja mtaani, zikakufuma risasi,
Hali huwa abautani, motoni na firdausi,
Ustaarabu gani wa ghorofa kwenye kinyesi?

Wakubwa tuwaombeeni, walione na wahisi,
Na maneno wasemeni, wajione na nuksi,
Wasijifiche mwao ndani, hali nje kiharusi,
Ustaarabu gani wa ghorofa kwenye kinyesi?

No comments: