Wednesday, October 12, 2011

Nyerere twakukumbuka

MBEGU iliyopandika, yenye za pekee sifa,
Tutakayoikumbuka, katika refu masafa,
Pasiwepo Tanganyika, kupata huu wadhifa,
Nyerere twakukumbuka, baba yetu wa taifa.

Kimwili umeondoka, ila kiroho hujafa,
Mengi uliyotamka, ni kubwa kwetu sahifa,
Na kila tukizinduka, twaitafuta sharifa,
Nyerere twakukumbuka, baba yetu wa taifa.

Ulihofia hakika, kujitokeza kwa nyufa,
Haya yamedhihirika, kabla kupiga chafya,
Na nchi wameishika, watu wasio na sifa,
Nyerere twakukumbuka, baba yetu wa taifa.

Fisadi wamejazuka, na tena wana wadhifa,
Imekuwa patashika, wazidiana maarifa,
Richmond aliposhuka, halikuhitaji khalifa,
Nyerere twakukumbuka, baba yetu wa taifa.

Kagoda wakamulika, faili lake kifafa,
Wengine wanaondoka, twakumbuka alfafa,
Dowans kuja kuzuka, haikuwa ni kashfa,
Nyerere twakukumbuka, baba yetu wa taifa.

Kulimbikiza wataka, hata walo na wadhifa,
Hisa kwenye mashirika, hivi leo si kashfa,
Lukuki wanalundika, mkoa hadi tarafa,
Nyerere twakukumbuka, baba yetu wa taifa.

Wanao hukuwaweka, kwenye yoyote nyadhifa,
Nyuma tunaweweseka, urithi sasa ni sifa,
Na wakubwa kupambika, kama mamisi hanifa,
Nyerere twakukumbuka, baba yetu wa taifa.

Bongo zinatatizika, hakuna mweye falsafa,
Insha wanaoandika, huzikwiba maarifa,
Kisha wakayapachika, ili wapate wao sifa,
Nyerere twakukumbuka, baba yetu wa taifa.

Nchi inatawanyika, imekosa makhalifa,
Dini zimeharibika, wamo wasio na sifa,
Wanasiasa wamechoka, na siasa zinakufa,
Nyerere twakukumbuka, baba yetu wa taifa.

Yashangaa Afrika, kurudi nyuma taifa,
Nchi ulipoishika, yalijaa maarifa,
Hivi leo twatishika, hakuna mwenye wasifa,
Nyerere twakukumbuka, baba yetu wa taifa.

Mwalimu umeondoka, ujamaa umekufa,
Ubepari wajengeka, usio na maarifa,
Wazawa tunateseka, na wengine hata kufa,
Nyerere twakukumbuka, baba yetu wa taifa.

Chama kimebadilika, usanii ni wadhifa,
Gamba gumu kujavuka, kofia zawachachafya,
Imani imetutoka, tunachongoja ni kufa,
Nyerere twakukumbuka, baba yetu wa taifa.

Badiliyo hatafika, karne hii ya mofa,
Heshima imeondoka, zasema taarifa,
Hata wetu washirika, wahoji kimataifa,
Nyerere twakukumbuka, baba yetu wa taifa.

Kalamu chini naweka, nikimwomba Raufa,
Busara kutoondoka, katika zote nyadhifa,
Na hekima kutukuka, katika hili taifa,
Nyerere twakukumbuka, baba yetu wa taifa.

No comments: