Tuesday, June 12, 2012

Dua mkubwa tabibu



Mkubwa tabibu dua, imani ikikujaa,
Hakuna usiloagua, watu wakatengenea,
Na  uzima kuingia, kwa wlaipokijifia,
Dua mkiziratibu nyingine ni mujarabu !

Natoa wangu usia, njiani kutoingia,
Huko watawaonea, na kusema mwavamia,
Toka lini linakuwa, liwalo kwenye mitaa ?
Dua mkiziratibu nyingine ni mujarabu !

Mambo kujatengenea, muhimu ukatulia,
Kila kitu kuwazia, na milango kuijua,
Ipi ni ya kufungua, na ipi ya kuondoa,
Dua mkiziratibu nyingine ni mujarabu !

Madirisha kung'amua, na wapi pa kutokea,
Kiakili nawambia, wala si kifizikia,
Na elimu naijua, ndo kwanza yatakiwa,
Dua mkiziratibu nyingine ni mujarabu !

Hili kulipalilia, hadi kilele kukwea,
Kisha ikafatia, ujasriamali kujua,
Na elimu kuenea, kiuchumi mkapaa,
Dua mkiziratibu nyingine ni mujarabu !

Viongozi wenye njaa, haya watayachezea,
Sadaka wanangojea, na kaizari kupewa,
Nadra wakaamua, mazuri yakuwafaa,
Dua mkiziratibu nyingine ni mujarabu !

Hao dini huziua, washikacho ni balaa,
Hata pasipo na njaa, lazima itaingia,
Ni nuksi na nazaa, katu hawatowafaa,
Dua mkiziratibu nyingine ni mujarabu !

Waja wanaosikiwa, ni kwa Mola zao dua,
Katu haijatokea, mtu kumuabudia,
Hilo watalikataa, na vyao pia kuvia,
Dua mkiziratibu nyingine ni mujarabu !

Halali hakitakuwa, haramu kilichokuwa,
Ukishika ni kinyaa, uoza utanukia,
Malaika hukimbia, hadi kinapoishia,
Dua mkiziratibu nyingine ni mujarabu !



No comments: