Sunday, June 17, 2012

Iwapo harufu mbaya



MAJENGO wajijengea, bustani zisokuwa,
Chini mashimo yajaa, na kinyesi kunukia,
Uchafuu unazagaa, kote ukiangalia,
Iwapo harufu mbaya, kila kitu kitanuka !

Uzuri unaovia, waenea Tanzania,
Maji yalikopotea, na mitaro ya balaa,
Usafi ulikofia, na maiti kubakia,
Iwapo harufu mbaya, kila kitu kitavia !

Huna utapoingia, kwenye ya umma mitaa,
Akili zikakwambia, hawa watu wamekuwa,
Ni unyama umejaa, kwa siha nayo afya,
Iwapo harufu mbaya, watu watatukimbia !

Amana waliopewa, sawasawa imekua,
Kipindupindu maua, yaachiwa kuchanua,
Wageni wajionea, na kumbukumbu kutia,
Iwapo harufu mbaya, kila kitu kitanuka !

Kurudi kwao nazaa, kueuka ya kinyaa,
Kwingine hujiendea, usafi wanakojua,
Ni miji ya majaliwa, kitu isiyojaliwa,
Iwapo harufu mbaya, kila kitu kitavia !

Majengo sasa yang'aa, ila miji yafubaa,
Usafi utaujua, ndani tu unapokuwa,
Nje kote ni balaa, ndio yetu Tanzania,
Iwapo harufu mbaya, watu watatukimbia !

Harufu inasambaa, hadi ndani kuingia,
Hadhari hatujajua, kukieneza kinyaa,
Imebaki mazoea, na watu wavumilia,
Iwapo harufu mbaya, kila kitu kitanuka !

Naimba sikuumbua, ukweli watu kujua,
Hali hii kuachiwa, twaelekea kubaya,
Watalii kukimbia, sifa mbaya kuenea,
Iwapo harufu mbaya, kila kitu kitavia !

Ila ninachokijua, usafi ni manufaa,
Ni huduma maridhawa, uchumi inanyanyua,
Usafi hununuliwa, mapesa yakaingia,
Iwapo harufu mbaya, watu watatukimbia !

Usafi unavutia, biashara zikakua,
Watu wakikuridhia, nyumbani kwako kukaa,
Wawekezi kuingia, mitaji wakaitoa,
Iwapo harufu mbaya, watu watatukimbia !

Uchafu ukizidia, hata nzi hukimbia,
Maafa yakaingia, ya maradhi na ukiwa,
Kidogo mlichopewa, hata nacho kupotea,
Iwapo harufu mbaya, watu watatukimbia !


No comments: