Tuesday, June 12, 2012

Hivi vijana wavivu ?



Hivi wavivu vijana, kuna mtu kanambia,
Naona kama wa jana, na wala hanayo haya,
Bongo makali hamna, kutu zimeshaingia,
Hivi vijana wavivu, au ajira ni kavu !

Nchi yakosa kuvuna, shamba haijafukua,
Wala hamna amana, mbegu za kujimwagia,
Wanaoula ubwana, vyumbani wajifungia,
Hivi vijana wavivu, au ajira ni kavu !

Nyote mngeandamana, fursa mngezitambua,
Mkafanya muamana, vitu vya kujifanzia,
Petu hapa kumenuna, ukubwa ni kujilia,
Hivi vijana wavivu, au ajira ni kavu !

Nani wa kuongozana, mkaonyeshana njia,
Kila mtu anabana, konani alimokuwa,
Kutoka nje utwana, wengi wanavyodhania,
Hivi vijana wavivu, au ajira ni kavu !

Sawa hawajapishana, ila kweli wakataa,
Ukubwa kweli utwana, na ukubwa pia baa,
Ukubwa kutumikana, na wala si kutumia,
Hivi vijana wavivu, au ajira ni kavu !

Karne hii nanena, mbali yatawafikia,
Watakuja soma wana, wajukuu kufwatia,
Wasiweze kupingana, haya zikawaindia,
Hivi vijana wavivu, au ajira ni kavu !

Yatakuja onekana, maana yake kujua,
Nami sintaonekana, wala sintowasikia,
Ila kwa yangu amana, ya wema niliotia,
Hivi vijana wavivu, au ajira ni kavu !

No comments: