Tuesday, June 12, 2012

Kuwanunua watu



Wangapi utanunua, posho wapi waitoa,
Hadi ukajipatia, cha macho kutia hadaa,
Ulimwengu wa kujua, kibaka wa kudokoa,
Huwezi ukanunua, watu wote Tanzania:
Za ufisazi zikisha !

Nafsi umechafua, kwa uchafu kuingia,
Na ubora wajitia, nayo hadhi usokuwa,
Mtu ungejichungua, haya ungeyakimbia,
Huwezi ukanunua, watu wote Tanzania:
Za ufisazi zikisha !

Wala tope haikuwa, hayo mavi yalikuwa,
Mabichi yakielea, miguuni yamejaa,
Harufu unaitoa, kila mtu akimbia,
Huwezi ukanunua, watu wote Tanzania:
Za ufisazi zikisha !

Mwalimu kaniandaa, kichafu kukikataa,
Hata changu kilokuwa, ukweli hukiambia,
Kwa wasionisikia, huruma huniishia,
Huwezi ukanunua, watu wote Tanzania:
Za ufisazi zikisha !

Mitume ninawajua, kwa wana na wake pia,
Wabora walizidiwa, usononi kuwajaa,
Mola alipowajua, dua zao kakataa,
Huwezi ukanunua, watu wote Tanzania:
Za ufisazi zikisha !

Hakifai kisichofaa, hata kwa watume pia,
Rehema kisichopewa, kilichojaa madoa,
Uchafu kujichimbia, usafi ukapotea,
Huwezi ukanunua, watu wote Tanzania:
Za ufisazi zikisha !

Huku mnawaibia, kule mkavitumia,
Mashimo mkachimbua, ya zamani kufukia,
Na nchi kuendelea, haiwezi ikatokea,
Huwezi ukanunua, watu wote Tanzania:
Za ufisazi zikisha !

Hilo nimelikataa, sitaki kuendelea,
Mbora namuangalia, na SIfaze kuzitoa,
Wabaya wakichukia, wema watafurahia,
Huwezi ukanunua, watu wote Tanzania:
Za ufisazi zikisha !


No comments: