Tuesday, June 12, 2012

Weupe watubagua

KOSA letu limekuwa, ni wao kuwategemea,
Watuona wenye njaa, ya kwao tunanbabia,
Vibaya tungejisikia, kwao tungelikimbia,
Weupe watubagua, kisa twawategemea !

Zamani ilivyokuwa, kila kitu kilijaa,
Leo wameelemewa, madeni  yawazidia,
Njaa yaanza ingia, na mgeni aonewa,
Weupe watubagua, kisa twawategemea !

Chakula mwawamalizia, kidogo kilichokuwa,
Na mashamba yamejaa, kama hapa Tanzania,
Mtapswa kurejea, maafa kuyakimbia,
Weupe watubagua, kisa twawategemea !

Ulaya yaugulia, kila mtu anajua,
Ila wanajihadaa, ukweli kuukimbia,
Wajifanza mashujaa, kumbe kitu wasokuwa,
Weupe watubagua, kisa twawategemea !

Nyumbani tukiamua, kuipiga vita n jaa,
Nchi ikaendelea, wazungu tuwanunua,
Watumishi wetu kuwa, mbona hili lajifia ?
Weupe watubagua, kisa twawategemea !

Mbumbumbu waliokuwa, ndio bora wadhania,
Sisi nao tulokaa, si kweli tunatambua,
Siku tukijifaragua, mizizi hawajajaliwa,
Weupe watubagua, kisa twawategemea !

Ila tusipojitambua, watazidi kutuvaa,
Wawe wanatuhadaa, kisiasa yao kuwa,
Hili tukiling'amua, mzungu saizi kawa,
Weupe watubagua, kisa twawategemea !

Kazi inayotakiwa, kwa mipango kujiandaa,
Bungeni mnapokuwa, ndoto kuizungumzia,
Uzushi hautofaa, kuweza mkajitia,
Weupe watubagua, kisa twawategemea !

Kuweza mkajitia, uzushi hautafaa,
Mengi hayajatimia, robo tatu natambua,
Ukweli tukiujua, huko tutakimbilia,
Weupe watubagua, kisa twawategemea !

Mbalimbali zatakiwa, njia zitakazotufaa,
Barabara kutanua, na reli kuifufua,
Viwanja vinatakiwa, maalum vilokuwa,
Weupe watubagua, kisa twawategemea !

Bandari zinatakiwa, meli kupumnzikia,
Na viwanja vyatakiwa, vya ndege pia kutua,
Nchi ikaendelea, kwa uchumi kuitembea,
Weupe watubagua, kisa twawategemea !

Mengi sana yatakiwa, uchumi kuupanua,
Haraka tena ikawa, wala si kwa kunyong'onyea,
Mwalimu katuusia, ni lazima kukimbia,
Weupe watubagua, kisa twawategemea !

No comments: