Tuesday, June 12, 2012

Alfajiri yaingia



Kuamka unatakiwa, wewe watafuta shuka,
Asubuhi imekua, na kengele yaropoka,
Kitandani kujitoa, uende mchakamchaka,
Alfajiri yaingia, ndio watafuta shuka !

Watakiwa kuachia, shukayo na kuondoka,
Na taulo kulitwaa, bafuni ukaingia,
Baridi kujiogea, upate kuchangamka,
Alfajiri yaingia, ndio watafuta shuka !

Hili afya hutia, japo kipupwe chawika,
Usiogope mafua, kifua haktachanika,
Ikiwa ni mazoea, huwezi kuathirika,
Alfajiri yaingia, ndio watafuta shuka !

Acha kuling'ang'ania, shuka lisije chanika,
Pugu ungeshaingia, mapema kunapitika,
Ndugu ukishachelewa, unaweza adhirika,
Alfajiri yaingia, ndio watafuta shuka !

Simu ninakupigia,mimi nimeshadamka,
Mjini ninaingia, na gazeti nimeshika
Mengi nimejisomea, jana yaliyosikika,
Alfajiri yaingia, ndio watafuta shuka !

No comments: