Tuesday, June 12, 2012

Imani ya kweli sumu



KILIO hukisikia, kwenye dua maalumu,
Mola ukimlilia, hasa kama madhulumu,
Ombi likaangaliwa, na adhabu kuazimu,
Imani ya kweli sumu, ukiomba unaua !

Usihofu kuonewa,na wengine binadamu,
Juu aliyetulia, yote anayafahamu,
Wakati ukitimia, na yao ikawa zamu,
Imani ya kweli sumu, ukiomba unaua !

Watu huwa wapotea, ukubwa nayo adhimu,
Ila si hii dunia, ambayo yajifahamu,
Nukta haitapotea, bila kujua kalamu,
Imani ya kweli sumu, ukiomba unaua !

Mtu usipotegemea, ukamjali hakamu,
Juu akatangulia, huupata ufahamu,
Chako hakitapotea, haki yako itadumu,
Imani ya kweli sumu, ukiomba unaua !

Vitu waweza chukua, lakini siyo kalamu,
Mbinguni itaingia, kwa heri kukusalimu,
Na kisha kuhadithia, rojo za wanaharamu,
Imani ya kweli sumu, ukiomba unaua !

Tena aone Karimu, haki kutoitangua,
Japo wewe ni hadimu, sultani unakuwa,
Dhulumati bila hamu, utumwa akaridhia,
Imani ya kweli sumu, ukiomba unaua !

'Siabudu wanadamu, hii si yao dunia,
Ikiisha yao zamu, patupu waambulia,
Liwe ni lako jukumu, imani kuiwania,
Imani ya kweli sumu, ukiomba unaua !

Ya kweli huwa ni sumu, ikawadhuru wabaya,
Pasipo kutakadamu, ya kwao kuingilia,
Wajikute milizamu, usoni waiachia,
Imani ya kweli sumu, ukiomba unaua !



No comments: