Tuesday, June 12, 2012

Wamekwishanunuliwa



Nini utatarajia, wakubwa 'kinunuliwa,
Mipango wakaundiwa, huyu, yule kumfaa,
Bei imeshaamuliwa, kwa gharama yoyote kua,
Wamekwishanunuliwa, wataka kuwanunua !

Hawa wakishanunuliwa, ni nani anabakia,
Funguo ukishafungua, mlango wazi unakuwa,
Kila kitu chaingia, na kutoka nako pia,
Wamekwishanunuliwa, wataka kuwanunua !

Tumaini lapotea, salama kujabakia,
Kuku kisu wametiwa, imebaki kunyonyoa,
Maji moto yatakiwa, nyama safi kubakia,
Wamekwishanunuliwa, wataka kuwanunua !

Njaa inawasumbua, hawajui kuchimbua,
Kazi yao kupakua, kama si kupakuliwa,
Hivyo ndivyo imekuwa, nini unategemea ?
Wamekwishanunuliwa, wataka kuwanunua !

Malipo waliopewa, mifukoni wamejaa,
Sasa wataka tumia, nasie kutununua,
Bei yetu watambua,  poa sana Tanzania,
Wamekwishanunuliwa, wataka kuwanunua !

Nchi inshanunuliwa, imebakia kuliwa,
Nani ananibishia, si kweli naongea ?
Masikini twajifia, kwa kiroho kutwingia,
Wamekwishanunuliwa, wataka kuwanunua !

Hadithi zasimuliwa, watu vitu kuchukua,
Wameishajigawia, wewe nini umepewa ?
Ni mitupu natambua, mikono ulozaliwa,
Wamekwishanunuliwa, wataka kuwanunua !

Huna la kushikilia, ulitunze na kukua,
Mitaji waibania, wenyewe ikawafaa,
Wake na wana pia, sio sisi wenye njaa,
Wamekwishanunuliwa, wataka kuwanunua !

Uchama sasa wavia, kuona tunatumiwa,
Wengine wajishibia, sisi hoi twabakia,
Hata na makombo pia, bei yake imepaa,
Wamekwishanunuliwa, wataka kuwanunua !

No comments: