Thursday, June 14, 2012

M W A N A M K E U S I M W I T E



Mwanamke mwite pusi, wito atausikia,
Atayafanza mepesi, magumu ulodhania,
Akatia udamisi, utakalo kujaliwa,
Mwanamke umwiite, pusi wala sio paka !

Ukimwita yeye paka, aweza kukurarua,
Makucha akakutia, viungo kukunyofoa,
Na meno akakutia, na nyama akaitoa,
Mwanamke umwiite, pusi wala sio paka !

Mwite mwanamke njiwa, hana budi kukujia,
Na begani akatua, la kwako kulisikia,
Huku tena asinzia, na macho kuyarembua,
Mwanamke umwiite, njiwa wala sio kuku !

Thubutu umwite kuku, kama hatokurukia,
Huruka huko na huku, akawa akudonoa,
Huwezi mfunga luku, mita zake hukimbia,
Mwanamke umwiite, njiwa wala sio kuku !

Mwanamke mwite toto, witowe atasikia,
Huenda ikawa ndoto, yake kwako ni ruia,
Na baridi kuwa joto, kwa ndani umetulia,
Mwanamke umwiite, toto ila si mtoto !

Ole, umwite mtoto, mawe  atakutupia,
Ukapata mkong'oto, na nundu kuzawadiwa,
Iwe ni yako majuto, neno kutokurudia,
Mwanamke umwiite, toto ila si mtoto !

Mwanamke mwite bonge, wala hatokuringia,
Huzubaa kama tonge, kinywani likichelewa,
Na shuleni mwenye nunge, uhodari kujaliwa,
Mwanamke umwiite, bonge wala si mnene !

Usimwiite mnene, hilo hatofurahia,
Mengine usiyanene, moyoni ataumia,
Nzige sio senene, kufanana haijawa,
Mwanamke umwiite, bonge wala si mnene !

Mwanamke mwite miss, kama mwembamba akiwa,
Huyo katu hakususi, cheo umempatia,
Atakuminya chunusi, na ndevu kuzichezea,
Mwanamke umwiite, 'kimisi' sio ukuni !

Ila njiti 'kimwambia, mbali nawe atakaa,
Moyoni kuugulia, Uzungu usikokuwa,
Biashara ikavia, mswahili kususia,
Mwanamke umwiite, 'kimisi' sio ukuni !

Mwanamke ni kijinga, mwana anayeutoa,
Kwa hayo ukimlenga, katu hatokuachia,
Wala tena hatoringa, yako unapomwitia,
Mwanamke umwiite, kijinga wala si mwanga !

Usije mwiita mwanga, daima hukuchukia,
Japo kajaliwa wanga, na azidi kuchakaa,
Yeye nuru sio mwanga, hawezi kukuelewa,
Mwanamke umwiite, nuru lakini si giza !

Mwanamke ni Chepe, hata Fataki ajua,
Hatolikosa la lepe, usingizi kumjia,
Roho ikawa nyeupe, kwa wito kuuridhia,
Mwanamke umwiite, cheupe wala si kupe !

Ukimwita yeye kupe, yako atakususia,
Hata vipi uongope, tena hautomrudia,
Hulipiga lake chepe, nasibu kuifukua,
Mwanamke umwiite, cheupe wala si kupe !

Ukimwiita bleki, uzuri hujisikia,
Masikini mamluki, lugha njema kudhania,
Akawa nayo ashiki, ya kwako kuyasikia,
Mwanamke umwiite, blaki sio mweusi !

Ni heri umwite cheuisi, kuliko awe mweusi,
Ataona ni nuksi, kiumbe kutojijua,
Akapunguza maksi, kwa kuutia  mkasi,
Mwanamke umwiite, blaki sio mweusi !

Mwanamke bwana jina, moyo utauchukua,
Ikawa yako amana, ndani umeichukua,
Pasiwe kwenye hiana, maisha kufurahia,
Mwanamke umwiite, jina wala si majina !

No comments: